Usalama kupewa kipaumbele Misri
13 Februari 2011Waziri Mkuu Ahmed Shafiq alitamka hayo kwenye televisheni baada ya kukutana na mkuu wa baraza la kijeshi Mohammed Hussein Tantawi. Alisema kuwa serikali ya mpito itatoa kipaumbele kurejesha utulivu. Vile vile alitoa mwito wa kuwepo umoja kati ya umma na serikali. Serikali ya mpito imeahidi kuanzisha mageuzi ya kidemokrasia na kuheshimu makubaliano ya kimataifa, ukiwemo mkataba wa amani uliotiwa saini pamoja na Israel tangu muda mrefu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali MENA, waziri mkuu wa zamani Ahmed Nasif na waziri wa habari wa hivi sasa Anas el Fekki wamepigwa marufuku kusafiri nje. Hata mali ya waziri wa zamani wa ndani Habib el Adli na familia yake imezuiliwa. Sababu ni tuhuma kuwa kampuni moja ya ujenzi imelipa kiasi ya Euro 500,000 katika akaunti ya Adli binafsi.
Rais Hosni Mubarak alijiuzulu kufuatia maandamano ya siku 18 na Wamisri wamesherehekea kuondoka kwake, huku wengine hiyo jana, wakijitolea kuusafisha uwanja wa Tahrir, kitovu cha vuguvugu la upinzani dhidi ya serikali.
Mwandishi: Prema Martin/afpe,rtre,dpae
Mhariri:Maryam Abdalla