Usalama wa ndani wazua majadiliano Ujerumani
9 Januari 2017Kuhusiana na mjadala wa usalama wa ndani nchini Ujerumani , mhariri wa gazeti la Rhein-Neckar-Zeitung la mjini Heidelberg anaandika:
Hali haionekani kabisa kuwa ni ya usalama wa kutosha. Kwasababu hakuna hadi sasa mwelekeo wa wazi, ambao ungewezekana kuzuwia shambulio dhidi ya soko la krismass mjini Berlin, iwapo vizuwizi vya saruji vilivyowekwa hivi sasa vitaondolewa. Kutumia hatua hizo anaona mhariri kuwa ni muhimu zaidi kuliko kuweka sheria mpya na mifumo. Ni vizuri basi kutumia sera zilizopo za usalama , pamoja na sheria zilizopo.
Gazeti la Landeszeitung la mjini Lüneburg likizungumzia kuhusu mada hiyo ya usalama wa ndani linaandika.
Baadhi ya wanasiasa hisia zao tayari ziko katika uchaguzi mkuu tu. Hali hiyo pia iko kwa wananchi wengi. Wanasiasa wameanza kujiingiza rasmi katika mjadala kuhusu shambulio la kigaidi mjini Berlin hususan katibu mkuu wa chama tawala CDU Peter Tauber Sahra Wagenknecht na Frauke Petry wakiwa ni watu wawili ambao wanapalilia siasa kali za mrengo wa kulia.Lakini wawakilishi hawa wa wananchi hawapaswi kushangaa , wakati ndugu za watu waliopoteza maisha na kujeruhiwa katika shambulio la mjini Berlin wanahisi kwamba wanasiasa wamewatupa kando. Tauber na wenzake wanapaswa hatimaye kutambua , kwamba siasa za kuwagawa wananchi ama siasa kali za mrengo wa kulia hazi katika mjadala huu.
Uchaguzi nchini Marekani
Kuhusu uchaguzi wa Marekani na udukuzi wa Urusi katika uchaguzi huo , mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung anaandika:
Ni kwa kiasi gani athari za wizi, udukuzi pamoja na wapi taarifa hizo za udukuzi zimepelekwa katika uchaguzi mkuu wa rais nchini Marekani zilichangia katika kubadilisha matokeo, ni suala ambalo haliwezi kupimwa. Lakini iwapo itaweza kuthibitishwa, kwamba nguvu kutoka nje zilichangia kuingilia kati mchakato wa kidemokrasia nchini Marekani, matokeo yake yanaonekana dunia nzima. Na kwa hakika hata Trump anaweza kumridhia Putin. Hakuna mtu ambaye angeweza bila shaka kukubali uhalali wa Trump. Iwapo kulikuwa na operesheni kama hiyo,bila ya kupata idhini kutoka juu, basi shirika la kijasusi la Urusi linapaswa kupongezwa kwa kazi ya mapinduzi lililofanya.
Smartphone:
Na simu za mkononi -Smartphone- zinatimiza miaka 10, mhariri wa gazeti la Der tagesspiegel anaandika.
Simu za mkononi za Smartphone ni msingi wa sekta mpya ya kiuchumi. Katika bara la Ulaya , baadhi ya watu wanajiuliza, iwapo chombo hicho kinawalazimisha watu kuingia katika utumwa wa kimamboleo na iwapo watu wanaweza kujiepusha nao. Katika nchi zinazoendelea simu hizo zimewaingiza watu wengi katika hali ya kujitegemea na kutatua matatizo halisi. Kwa kutumia app wakulima wadogo wadogo wameweza kujifunza masuala ya kilimo, na kuweza kuweka mashamba yao katika hali bora zaidi. Wafugaji wameweza kulipa malipo yao ya bima ya majanga kupitia simu zao za mkononi, wakati ukame ukiwa umeendelea kwa muda mrefu. Iwapo watu wanakabiliwa na njaa katika maeneo kame, wameweza kutuma taarifa kwa serikali ili kupata msaada kupitia simu zao za mkononi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse
Mhariri: Yusuf Saumu