Usalama waimarishwa kueekea uchaguzi Zimbabwe
30 Julai 2013Kulingana na televisheni ya kitaifa nchini humo maelfu ya maafisa wamepelekwa katika eneo la katikati mwa mji na mikoani huku magari yaliokuwa yamebeba silaha yakionekana kupiga doria katika miji ya Harare na Mbare.
Maeneo ambayo maafisa polisi walikuwa wanapiga doria ni maeneo yalio na wafuasi wengi wa waziri mkuu Morgan Tsvangirai na ambayo pia yalishuhudia ghasia katika uchaguzi wa 2008 ambako watu 200 wa chama cha MDC cha waziri mkuu waliuwawa.
Uchaguzi wa mwaka huu wa urais pamoja na bunge unanuiwa kumaliza miaka minne ya uongozi wa serikali ya muungano kati ya Rais Robert Mugabe wa chama cha ZANU-PF na Morgan Tsvangirai wa chama cha MDC.
Huku kukiwa hakuonekani hali ya kuaminika ni vigumu sana kueleza iwapo Tsvangirai aliye na umri wa miaka 61 atafanikiwa kweli katika juhudi zake za kumuondoa madarakani rais wa sasa Robert Mugabe aliye na umri wa miaka 89 ambaye ameiongoza nchi hiyo kuanzia ijipatie uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka wa 1980.
Uchaguzi kufanyika Jumatano
Hata hivyo waangalizi wa kura wa nchi za Magharibi wamepigwa marufuku ya kufuatilia uchaguzi huo na kazi hiyo kupewa waangalizi 500 wa kanda na wengine 7000 wa ndani ya nchi. Matokeo ya rasmi uchaguzi yanatarajiwa kutolewa baada ya siku tano lakini huenda pia yakajulikanamapema.
"Mugabe ni mmoja wa viongozi wakongwe duniani na tena ni mmoja wa madikteta wanaotawala anajaribu kutumia mbinu nyengine ya kuiba kura kuliko ile iliotumiwa na ZANU-PF katika kampeni zake zilizopita," alisema Morgan Tsvangirai
Siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi chama cha upinzani kimetoa ushahidi kwa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika unaonesha chama tawala kinapanga njama za kuiba kura.
Hata hivyo akizungumza na waandishi habari nchini humo Rais Robert Mugabe amesema ataachia ngazi iwapo atashindwa katika uchaguzi. Mugabe ameiongoza Zimbabwe kwa miaka 33.
Mwandishi: Amina Abubakar
Mahriri: Mohammed Abdul-Rahman