1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushahidi: China inawafunga Wauighur bila sababu za msingi

Sylvia Mwehozi
18 Februari 2020

Nyaraka mpya zilizovuja zinadhihirisha namna China inavyowafunga Waislamu wa jamii ya wachache wa Uighur kutokana na sababu zisizo za msingi zinazohusiana na dini na tamaduni zao.

DW Investigativ Projekt: Uiguren Umerziehungslager in China ACHTUNG SPERRFRIST 17.02.2020/17.00 Uhr MEZ
Picha: AFP/G. Baker

DW imezungumza na ndugu wa baadhi ya Wauighur ambao wamepotelea katika makambi ya kutoa mafunzo. Mnamo Mei 2017, mwanaume mmoja wa jamii ya Uighur alichukuliwa na kupelekwa kwenye "kambi ya kutowa elimu" kwenye mkoa wa kaskazini magharibi mwa China wa Xinjiang. Kama Muislamu alisali nyumbani kwake na wakati mwingine kuhudhuria ibada katika msikitiki wa karibu. Mke wake alifunika vyema kichwa chake na ushungi na walizaa watoto wengi. Hizi zilikuwa ni sababu za kukamatwa kwake na kupelekwa kwenye hayo makambi ingawa hapakuwa na kesi ya aina yoyote.

Moja ya kambi wannamoshikiliwa watu wa jamii ya UighurPicha: AFP/G. Baker

Hadithi yake inafanana na mamia ya kesi zilizoorodheshwa zikiambatana na maelezo ya kushangaza. Nyaraka hizo zinatoa taarifa za kwanini watu wanakamatwa, wakati zikibainisha jinsi mamlaka za China zinavyotumia teknolojia ya kiwango cha juu kuwafutilia katika maeneo waliko na mienendo ya waislamu hao wa jamii ya Uighur.

Orodha ya wale waliofungwa imeelezea hatma ya watu 311, ambao walipelekwa kwenye "kambi za kutoa elimu" kati ya mwaka 2017 na 2018 kutokana na sababu zisizo na msingi kama kufuga ndevu, kufunga au kuomba pasipoti.

Uchambuzi uliofanywa na DW, kwa kushirikiana na mashirika ya utangazaji ya Ujerumani NDR na WDR na gazeti la Süddeutsch Zeitung, unachora taswira ya kile ambacho mashirika mengi ya haki za binadamu yanahofia kuwa ni kampeni ya ubaguzi wa kikabila na kufungwa kiholela kinyume na sheria. Ni vigumu kusema ni watu wangapi wamefungwa ingawa inakadiriwa kuwa karibu watu milioni moja wa jamii hiyo ya Uighur wanaoishi mjini  Xinjiang wamepotelea katika mtandao wa magereza na makambi.

Ripoti kutoka mkoa huo zinaonyesha kwamba baadhi ya wafungwa wanashikiliwa maisha, wengine wamehamishiwa katika kambi za kufanya kazi na wale wanaoruhusiwa kurudi nyumbani wanasalia katika ufuatiliwaji mkubwa huku uhuru wa kutembea ukiwa na mipaka.

Mlinzi akiwa kwenye mnara uliopo kwenye kambi zinazodaiwa kutoa elimuPicha: Reuters/T. Peter

Mwaka 2014, mamlaka za Chinazilianzisha mfumo wa ufuatiliaji na vituo vikubwa vya vizuizi, baada ya mripuko wa bomu la kujitoa muhanga kwenye jimbo la Xinjiang. Chama cha kikomunisti cha China kinauita mfumo huo kuwa mfumo wa hiari wa elimu ya ufundi na kwamba ulibuniwa mahususi kwa ajili ya kukabiliana na "itikadi kali" na kuwapatia Wauighur "maarifa ya maana".

Nyaraka hizo zilizo na kurasa 137 zimeeleza kila hatua mjini Xinjiang kuwa inafuatiliwa na kamera za usalama na teknolojia ya utambuzi wa uso sambamba na Apps za lazima kwenye simu.  Kesi zote hizo zilizoorodheshwa ni za Wauighur wa kutoka kaunti ya Karakax, iliyoko eneo la Hotan Prefecture huko kusini magharibi mwa Xinjiang karibu na mipaka ya India na Tibet.