Ushahidi wamhusisha bin Salman na kifo cha Khashoggi
19 Juni 2019Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa Agnes Callamard amependekeza ufanyike uchunguzi juu ya uwezekano wa ushiriki wa mwanamfalme Mohammed bin Salman katika mauaji hayo, akisema upo ushahidi wa kuaminika kumhusisha mrithi huyo wa ufalme na mauaji ya Khashoggi.
Madai kuhusu uwezekano wa jukumu la moja kwa moja la mrithi wa kiti cha ufalme Mohammed bin Salman katika mauaji ya Khashoggi Oktoba mwaka uliopita, yamebainishwa kwa kina katika ripoti mpya iliyotolewa siku ya Jumatano mjini Geneva, nchini Uswisi.
Ripoti hiyo yanye kurasa 101 juu ya mauaji ya Khashoggi kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki, inatoa mwito kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa au Katibu Mkuu Antonio Guterres, kufungua uchunguzi zaidi wa uhalifu.
"Kuna ushahidi imara na wa kuaminika kwamba eneo la uhalifu siyo tu lilichunguzwa, lakini pia lilisafishwa, kiasi kwamba kufikia wakati wachunguzi wa Uturuki walipoweza kuingia ubalozi, walikuta karibu kila kitu kimeondolewa," alisema mchunguzi maalumu Agnes Callamard.
Aliongeza kuwa wachunguzi wa Uturuki wameainisha uwezekano kwamba ushahidi mwingi ulikuwa umesafishwa.
Ushahidi wa kuaminika dhidi ya mrithi wa Mfalme
Khashoggi, aliekuwa mchangiaji wa gazeti la Washington Post na mkosoaji wa mwanamfalme Mohammed, aliuawa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul Oktoba 2. Awali serikali mjini Riyadh ilisema haikujua chochote kuhusu hatma yake.
Baadae ikawalaumu mawakala iliyowataja kuwa wahalifu kwa mauaji yake ndani ya ubalozi huo. Waendesha mashtaka wa Saudia wamemuondolea lawama mwanamfalme katika sakata hilo.
Lakini Callamard amesema uchunguzi wake umebaini kwamba kuna ushahidi wa kuaminika, unaoruhusu uchunguzi zaidi wa maafisa wa ngazi ya juu wa Saudi Arabia, akiwemo mrithi wa ufalme.
"Nilichonacho ni ushahidi unaoonyesha kuhusika kwa maafisa wa ngazi ya juu na hivyo kuhitaji uchunguzi zaidi, hasa dhidi ya mrithi wa ufalme kwa sababu mbalimbali, na kubwa kabisaa kwa kuwa watu waliohusika na mauji hayo waliripoti kwake moja kwa moja."
Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa kufuatia mauaji ya Kashoggi vimeshindwa kushughulikia masuala makuu ya mnyororo wa uongozi na wajibu wa maafisa wa juu uongozini kuhusiana na mauaji hayo.
Uturuki yaunga mkono wito wa kucgunguzwa bin Salman
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema Ankara inaunga mkono kwa nguvu wito kwa Umoja wa Mataifa kumchunguza mwanamfalme Salman na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa Saudi Arabia kuhusiana na mauaji ya Khashoggi.
"Tunaunga mkono ushauri wa Umoja wa Mataifa ili kutoa mwangaza juu ya mauaji ya Khashoggi na kuwawajibisha waliohusika," Cavusoglu alisema katika matamshi yaliochapishwa na shirika la habari la Uturuki Anadolu.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,afpe,afptv
Mhariri: Sekione Kitojo