Ushawishi wa Jumuiya ya madola watiliwa shaka
18 Novemba 2013Sri Lanka ilitarajia kuwa mkutano huo wa kilele wa siku tatu mjini Colombo ungeweza kuwa jukwaa muafaka la kuonyesha hatua ilizozipiga kujikwamua baada ya vita vya muda mrefu huku jumuiya ya madola ikitaka kuangazia ukuaji sawa wa kiuchumi na kuziondolea mzigo wa madeni wa nchi ndogo wanachama miongoni mwa masuala mengine.
Badala yake, mkutano huo ulizongwa na mzozo wa hadharani kati ya waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na Rais wa Sri Lanka Mahinda Rajapakse kuhusiana na madai kuwa majeshi ya Sri Lanka yaliwaua kiasi ya raia 40,000 mwishoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 37.
Je bado jumuiya ya madola ina manufaa?
Wachambuzi wanauona mkutano huo haukuwa na mafanikio yoyote.Ronald Sanders mwanadiplomasia wa zamani kutoka Guyana ambaye sasa ni mtafiti mwandamizi katika chuo cha mafunzo chajumuiya ya madola mjini London amesema hakuna mkutano unaotawaliwa na mivutano miongoni mwa wanachama kuhusu chaguo la Sri Lanka kuwa mwenyeji na uenyekiti ambao unaweza kutajwa kuwa wa mafanikio.
Sanders ambaye alikuwa miongoni mwa wataalamu waliokuwa wakikusanya mapendekezo ya kuwa na mchakato wa ruwaza ya pamoja ya nchi wanachama wa jumuiya ya madola anasema badala yake imeidhoofisha jumuiya hiyo.
Viongozi wa Canada,India na Mauritius waliususia mkutano huo unaofanywa kila baada ya miaka miwili ili kupinga rekodi tete ya Sri Lanka ya haki za binadaamu hasa dhidi ya walio wachache kutoka kabila la Tamil.
Viongozi walumbana kuhusu rekodi ya Sri Lanka
Waziri mkuu wa Uingereza ndiye alionekana kugonga vichwa vya habari kwa kutishia mara kwa mara kuanzisha uchunguzi wa kimataifa kupitia mashirika mbali mbali ya umoja wa Mataifa kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo la sivyo serikali ya Rajapakse ikamilishe uchunguzi wake ifikapo mwezi Machi mwakani.
Cameron alitembelea eneo lililokumbwa na mzozo la Jaffna kutilia msisitizo hilo na kuondoka nchini humo kabla ya hata mkutano huo wa jumuiya ya madola haujakamilika.
Rajapakse kwa upande wake alionya hatashinikizwa kuhusiana na suala hilo huku vyombo vya habari nchini Sri Lanka ambavyo vingi vyao vinaunga mkono serikali vikisema vitisho vya Cameron vinaashiria ubabe wa ukoloni.
Licha ya kuwa suala hilo la rekodi ya Sri Lanka kuhusu haki za binadamu ndilo lililotawala katika mkutano huo,taarifa ya pamoja kutoka viongozi wa mkutano huo wa jumuiya ya madola iliyotolewa hapo jana haikulitaja hilo na badala yake kusisitiza kujitolea kwa nchi hizo 53 wanachama ambazo nyingi walikuwa chini ya Uingereza wakati wa enzi ya ukoloni kuzingatia ajenda yao ya pamoja ambayo inajumuisha haki za binadaamu,demokrasia na utawala unaoheshimu sheria.
Jumuiya hiyo iliyoundwa miaka 64 iliyopita ikiwa na chimbuko lake kutoka uongozi wa kifalme wa Uingereza,imekuwa kwa muda mrefu sasa ikishutumiwa kuwa inatapatapa kusalia na ushawishi katika karne ya 21.
Mwandishi:Caro Robi/Afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman