1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushawishi wa Kabila, Bemba na Katumbi katika siasa za DRC

25 Desemba 2018

Wachambuzi wengi wana mashaka ikiwa rais Kabila ataacha siasa. Wanabashiri kuwa atakuwa na ushawishi mkubwa wa chini kwa chini, na mbinu hiyohiyo pia huenda ikatumiwa na Pierre Bemba pamoja na Moise Katumbi.

Kongo: Bildkombo Moise Katumbi und Jean-Pierre Bemba

Uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaotarajiwa kufanyika tarehe 30 Desemba bila shaka utaufikisha mwisho utawala wa rais Joseph Kabila ambaye ameiongoza nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini lkwa takriban miaka 18 lakini kongo inakumbwa na misukosuko. Rais Joseph Kabila, Jean-Pierre Bemba na Moise Katumbi, hawagombei urais lakini wana ushawishi mkubwa.

Ikiwa uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC utafanyika Jumapili tarehe 30, basi itakuwa mara ya kwanza kwa nchi hiyo kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani baada ya ukoloni.

Lakini wachambuzi wengi wana mashaka ikiwa rais Kabila ataacha siasa na badala yake wanabashiri kuwa atakuwa na ushawishi mkubwa, mbinu ambayo pia huenda ikatumiwa pakubwa na wapinzani wake wawili, muasi wa zamani Jean-Pierre Bemba na Moise Katumbi aliyeko uhamishoni.

Rais Joseph Kabila aliiingia madarakani akiwa na umri wa miaka 29 baada ya baba yake aliyekuwa rais wa Kongo Laurent-Desire kuuawa na mlinzi wake mnamo mwaka wa 2001.

Rais Joseph Kabila ana umri wa miaka 47 na ameiongoza DRC kwa miaka 18.Picha: Reuters/K.Katombe

Ikiwa uchaguzi ambao umeahirishwa sasa kwa mara ya tatu utafanyika kulingana na mipango, basi kabila ataondoka madarakani na kuchukua nafasi ambayo marais wa zamani wa nchi hiyo hupewa ambayo ni kuwa seneta wa kudumu.

Akiwa na umri wa miaka 47, Rais Kabila hajaweka wazi mustakabali wake na hata huonekana kutokuwa na mpango wa kustaafu.

Wakati mmoja Rais Kabila aliwaambia waandishi wa vyombo vya kimataifa kuwa "sawa na katika maisha, katika siasa pia siwezi kusema la kwa chochote." Alisema mustakabali wake kisiasa unaweza kueleweka wazi ifikapo mwaka wa 2023, ambapo nchi hiyo inatarajiwa kufanya uchaguzi mwingine wa rais.

Wakosoaji wanasema Kabila anapanga kuendelea kuongoza kupitia mrithi aliyemteua mwenyewe, waziri wa zamani wa ndani ya nchi hiyo, Emmanuel Ramazani Shadary anayegombea urais kwa tiketi ya chama tawala.

Baada ya miaka 18 madarakani, Kabila pia amejijengea mtandao wa wapambe katika jeshi na vyombo vya usalama na chombo kitiifu kwake kisiasa, muungano maalum kwa Wakongomani- Common Front for Congo (FCC).

Martin Fayulu, mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa vyama vya upinzani DRCPicha: Reuters/S. Mambo

Kabila ana ushawishi mkubwa katika uchumi wa nchi hiyo. Utafiti wa Bloomberg uliofanywa miaka miwili iliyopita ilibaini kuwa familia ya Kabila imejijengea mtandao mkubwa wa kibiashara kote DRC.

Kiongozi wa zamani wa waasi Jean-Pierre Bemba mwenye umri wa miaka 56 amekuwa mwanasiasa mzoefu katika siasa za DRC na pia ni mshindani mkubwa wa Kabila kwa miaka mingi.

Bemba ana uungwaji mkono mkubwa hasa Kaskazini magharibi mwa DRC. Maelfu kwa maelfu ya wafuasi wake walijitokeza kumlaki aliporudi nchini humo mwezi Agosti.

Sawa na Moise Katumbi, Bemba ambaye amezuiliwa kuwania urais, pia anamuunga mkono mgombea urais asiyejulikana sana Martin Fayulu, ambaye ni mkurugenzi wa zamani wa shirika la mafuta.

Licha ya kuzuiliwa kuwania urais, tajiri Moise Katumbi mwenye umri wa miaka 53 angali anaweza kuwa na ushawishi kuhusu mstakabali wa DRC kwa kumuunga mkono Fayulu.

Mhariri: Zainab Aziz

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW