Ushindi wa kishindo wa wahafidhina Uingereza
13 Desemba 2019"Serikali ya kihafidhina ya nchi hii imepatiwa madaraka makubwa zaidi ya kukamilisha mchakato wa Brexit. Na sio tu kukamilisha mchakato wa Brexit bali pia kuiunganisha nchi yetu na kutanguliza mbele mahitaji muhimu ya Waingereza."
Amesema hayo waziri mkuu Boris Johnson mara baada ya kuthibitika ushindi wa chama chake cha kihafidhina Tories. Boris Johnson amepania anasema kuitoa Uingereza katika Umoja wa ulaya hadi ifikapo january 31 mwaka 2020. Amewashukuru wote wale waliokipigia kura kwa mara ya kwanza chama cha kihafidhina na kukisaidia chama chake kujipatia wingi mkubwa wa viti bungeni."Mmetupatia kura zenu bila ya kujali kuwa nyie si wahafidhina" amesema Boris Johnson baada ya idadi isiyo ndogo ya wafuasi wa chama cha upinzani cha Labour kukipigia kura chama hicho cha kihafidhina.
Mwenyekiti wa chama hicho cha upinzani, Jeremy Corbyn amesema hatogombea tena wadhifa huo kufuatia pigo la uchaguzi mkuu wa jana.
Uingereza na Marekani wako huru kufikia makubaliano mepya ya biashara
Pongezi kwa ushindi wa chama cha kihafidhina zimetumwa na viongozi kadhaa wa dunia. Rais wa Marekani Donald Trump anasema katika salam zake za pongezi ushindi wa Johnson unamaanisha Uingereza na Marekani zitakuwa huru "kufikia makubaliano mepya ya biashara baada ya Brexit."
Viongozi wa Umoja wa ulaya wameupongeza pia ushindi wa Boris Johnnson na kutoa wito wa kupigiwa kura haraka na bunge la nchi hiyo mchakato wa kujitoa Uingereza katika Umoja wa ulaya. Hata hivyo waziri mkuu wa jamhuri ya Cheki anaonya ushindi wa Boris Johnson "ni habari mbaya kwa ulaya."Ameshinda na sasa kwa bahati mbaya watatoka" amesema waziri mkuu Andrej Babis.
Mwenyekiti wa baraza la Ulaya Charles Michel amempongeza kwa upande wake Boris Johnson na kusema Umoja wa ulaya uko tayari kujadiliana kuhusu makubaliano ya biashara huru lakini amekwepa kusema kama makubaliano hayo yanaweza kufikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja.