1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushindi wa Rais Robert Mugabe sasa watiliwa shaka

MjahidA9 Agosti 2013

Huku Kamishna wa pili katika tume ya uchaguzi ya Zimbabwe akijiuzulu vyama vya upinzani pamoja na wanaharakati wamenza sasa kutilia shaka uhalali wa matokeao yaliompa ushindi Rais Robert Mugabe katika uchaguzi Uliopita.

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe
Rais wa Zimbabwe Robert MugabePicha: Reuters

Kujiuzulu kwa Profesa Geoff Feltoe siku ya Jumanne kumekuja wakati kamishna mwengine wa tume hiyo ya uchaguzi nchini Zimbabwe Mkhululi Nyathi pia akijiuzulu.

Nyathi alijiuzulu Julai 31 siku ya uchaguzi wenyewe akisema anachukua hatua hiyo kutokana na kutofurahishwa na namna uchaguzi ulivyoeendeshwa.

Kamishna huyo amesema kujiuzulu kwake pia kunatokana na tume ya uchaguzi kushindwa kuhakikisha uhalali wa shughuli nzima ya uchaguzi.

Kuta zilizo na nembo ya Rais Mugabe na Morgan Tsvangirai wakati wa KampeniPicha: Reuters

Feltoe, afisa wa pili aliyejiuzulu, hadi sasa hajatoa sababu ya kufanya hivyo lakini afisa mmoja mkuu wa upande wa upinzani aliliambia shirika la habari la IPS kuwa huenda kamishna huyo wa pili akawa amejiuzulu kwa sababu sawa na za kamisha wa kwanza.

Ushindi wa Mugabe watiliwa shaka

Rais Robert Mugabe wa chama tawala cha ZANU-PF alinyakuwa ushindi katika uchaguzi uliomalizika hivi maajuzi nchini Zimbabwe, kwa kujipatia asilimia 61 ya kura, huku mpinzani wake Morgan Tsvangirai wa chama cha MDC akipata asilimia 34 ya kura. Takriban wazimbabwe milioni 3.4 walipiga kura.

Hata hivyo ushindi mkubwa wa Robert Mugabe uliwafanya wanaharakati pamoja na wachambuzi kujiuliza ni vipi Rais huyo amepata uungwaji mkubwa wa watu ikizingatiwa kwamba aliipelekea kukuwa kwa mfumuko wa bei nchini humo mwaka wa 2008.

Rais Mugabe na Mpinzani wake Morgan TsvangiraiPicha: AP

Huku hayo yakijiri upande wa tume ya uchaguzi imeripoti kwamba katika zoezi la uchaguzi takriban wapiga kura laki tatu walirudishwa bila ya kushiriki zoezi hilo.

Kwa upande mwengine upinzani umesema na wengine zaidi ya lakini mbili walipata msaada wa kupiga kura kutoka kwa maafisa wa uchaguzi.

Chama cha MDC chawasilisha kesi Mahakamani

Kuna ripoti pia juu ya kutishiwa kwa wapiga kura kutoka kwa wafuasi wa chama cha ZANU-PF lakini hata hivyo hakukuwa na ripoti zozote juu ya ghasia katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Sasa chama cha MDC kimepanga kufika mahakamani hii leo kupinga matokeo yaliompa ushindi Robert Mugabe. Kuwasilishwa kwa kesi hii mahakamani huenda ikachelewesha kuapishwa kwa Mugabe kama rais wa nchi hiyo kwa muhulu wa saba.

Mkuu wa chama cha Upinzani Morgan TsvangiraiPicha: Alexander Joe/AFP/Getty Images

Mahakama kuu nchini humo itakuwa na siku 14 ya kutoauamuzi wake. Kulingana na msemaji wa chama hicho Douglas Mwonzora iwapo hawataona haki ikitendeka katika kesi hii wanayoiwasilisha katika mahakama kuu, watasonga mbele na kuipeleka kwa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika SADC. Kimsingi Rais Robert Mugabe anapaswa kuapishwa siku ya Jumatano wiki ijayo.

Mwandishi: Amina Abubakar/IPS/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi