WHO: Ushirikiano wenye nia ya kudhibiti Corona kutangazwa
24 Aprili 2020Mkurugenzi wa WHO, Tedros Adhanom Gebreyesus amesema msisitizo pia utawekwa katika kuzitengeneza chanjo hizo na kuwezesha kupatikana kwa yoyote anayehitaji kote ulimwenguni. Aprili 6, Gebreyesus alipotangaza kuhusu mpango huo alisema hakutakuwepo na ubaguzi wa upatinaji kati ya aliyenacho na asiyenacho.
Mkuu wa shirika la haki za binadaamu katika Umoja wa Mataifa Michelle Brachelet amekosoa mataifa yaliyoutumia mzozo wa virusi vya corona kama sababu ya kuwakamata waandishi wa Habari na kuzuia utoaji wa taarifa.
Brachelet amesema huu sio wakati wa kumlaumu mjumbe, na kusema vyombo vya Habari ni muhimu wakati wote, lakini hakuna wakati ambapo jamii inavitegemea zaidi, kuliko sasa.
Nchini Ujerumani, shirika la habari la DPA limeripoti kwamba jimbo la Bavaria litaanzisha faini ya hadi Euro 5,000, kwa watakaokiuka sheria ya kuvaa barakoa. Faini kubwa zaidi itawahusu wamiliki wa maduka watakaoshindwa kuhakikisha kwamba watumishi wao hawazibi midomo na pua.
Watu wanaotumia usafiri wa umma na wanaofanya manunuzi, ambao hawatavaa barakoa watapigwa faini ya hadi Euro 150, sawa na karibu shilingi 350,000 ya kitanzania.
Trump apingwa.
Huko nchini Ufaransa, wataalamu wamepuuzilia mbali ushauri waliouita wa kipuuzi wa rais Donald Trump wa Marekani wa kuwatibu wagonjwa wa COVID19 kwa kuwachoma dawa ya kuua vijidudu ama disinfentant.
Madaktari na wataalamu wa afya wamesema kwenye mahojiano na kwenye mitandao ya kijamii kwamba mtizamo huo wa kuwaingizia mwilini wagonjwa aina yoyote ya bidhaa za kusafishia ni wa kipuuzi na wa hatari, kama alivyonukuliwa daktari bingwa wa magonjwa yanayoshambulia mapafu Vin Gupta alipozungumza na kituo cha Habari cha NBC News.
Waendesha mashitaka nchini Ugiriki wameanzisha uchunguzi kuhusu iwapo kuna uwezekano wa kufunguliwa mashitaka ya uhalifu dhidi ya menejimenti ya kliniki mbili binafsi zilizopo mjini Anthens baada ya idadi kubwa ya watumishi wake kuambukizwa virusi vya corona.
Ni hatua inayoangaziwa wakati mamlaka za afya zikiendelea kuchukua vipimo huku kukiwa na hofu ya ongezeko la idadi ya walioathirika. Msemaji wa wizara ya afya Sotiris Tsiodras amesema uzembe wa kuchukua tahadhari unachochea maambukizi mapya, baada ya jana kuripoti visa vipya 55, 28 vikitokea kwenye kliniki moja.
Na huko Japan, meya wa jiji la Osaka amejikuta mashakani na kukabiliwa na ukosoaji baada ya kushauri wanaume kufanya manunuzi katika kipindi hiki, badala ya wanawake ili kuwanusuru wanawake ambao hufanya maamuzi taratibu na huchukua muda mrefu madukani. Japan imetangaza hali ya dharura kutokana na janga la corona
Vyanzo: AFP|DPA|AP|Reuters|DW