1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usimamizi mbaya, uhaba wa wahudumu chanzo maafa ya Pumwani

Shisia Wasilwa
19 Septemba 2018

Kamati ya Seneti nchini Kenya imegundua kuwa kukosekana kwa usimamizi mzuri na wahudumu wa kutosha wa afya kulichangia mkasa wa maiti 11 za watoto wachanga kukutwa kwenye maboksi katika hospitali moja nchini humo.

Nairobi - Mike Sonko nach Stimmabgabe
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Uozo katika hospitali ya Pumwani unachora taswira pana ya jinsi sekta ya afya nchini Kenya inavyokabiliwa na changamoto licha ya kutengewa shilingi bilioni 90 huku jimbo la Nairobi likipokea mgao wa shilingi bilioni 15 - kiwango kikubwa cha fedha kutoka kwenye bajeti kuu.

Kadhia ya maiti 11 za watoto kupatikana zikiwa zimefungwa kwenye karatasi za plasitiki kisha kuhifadhiwa kwenye masandaku, iliilazimisha kamati ya seneti kuhusu afya, usalama  na ugatuzi kuzuru hospitali hiyo kujionea hali halisi; na ugunduzi wao unaacha maswali mengi zaidi kuliko majibu kwani tangu ilipoanzishwa mwaka 1921, hadi sasa haina chumba cha kuhifadhia maiti.

"Ni bayana kama usiku na mchana kwamba kuna tatizo la uongozi. Ukienda mahali tumekuwa mahali kuna jaa la takataka, mara ya mwisho liliposhughulikiwa ni miezi mitatu iliyopita. Tumeambiwa kuwa mtu ambaye hufanya usafi mahali pale, wakati mwengine amepata watoto wachanga waliokufa kwenye jaa hilo," alisema Seneta Jonson Sakaja wa Nairobi.

Aidha, kamati hiyo ya seneti imegundua kuwa hali kwenye chumba cha kuwalaza watoto wachanga ni ya kuhuzunisha na sasa inapanga kufanya mazungumzo na Gavana Mike Sonko wa Nairobi kuhusu jinsi anavyosimamia masuala ya afya jijini. Ni gavana huyo ndiye ambaye mwanzoni mwa wiki alilizusha suala hili baada ya kutembelea hospitali hiyo. Kamati hiyo ilisema ingelifanya kikao na madaktari kuweka mikakati ya kuimarisha hospitali hii.

"Ukiangalia watu wanaotembelea hospitali yenyewe na miundombinu iliyoko kwenye hospitali yenyewe, inaonekana iko nyuma kidogo. Kwa hivyo ni lazima tuongeze majengo kwenye hospitali zetu, tukifuatilia zile ajenda nne ambazo serikali imeweka," alisema John Kinywa, mwenyekiti wa Kamati ya Ugatuzi kwenye Seneti.

Utaratibu wa kuhamisha maiti wazorota

Hapo kabla, maiti za watoto na kina mama zilikuwa zinakusanywa kila siku na kupelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha City, lakini siku hizi huwa zinakusanywa Jumatatu, Jumatano na Ijumaa. Hospitali hiyo inasema kuwa maiti za watoto zilizopatikana na Gavana Sonko kwenye ziara ya kushtukiza zilikuwa za siku tatu. Hatua ambayo ilimlazimisha gavana huyo kuwafuta kazi madaktari watatu na kuvunja bodi ya hospitali hiyo.

Hata hivyo, hatua hiyo haikuchukuliwa vyema na Muungano wa Madaktari nchini Kenya, ambapo katibu wa muungano huo tawi la Nairobi, Dk. Alex Thuranira, aliiambia DW kwamba ni lazima madaktari hao warejeshwe kazini.

"Msimamo wetu ni kuwa tutasimama kidete, madaktari lazima warudishwe kazi na wasiporudishwa tutachukua hatua yoyote, tunaweza kuenda mahakamani ama kufanya mgomo. Kesho tutakuwa na mkutano kuwaambia jinsi tunataka sekta ya afya iendeshwe, hatutakaa tukitukanwa kila siku."

Hospitali hiyo, ambayo ndiko alikozaliwa Rais Uhuru Kenyatta miaka 56 iliyopita, imekanusha kuwa vifo vya watoto hao vilichangiwa na uzembe. Baada ya mkasa huu, Gavana Sonko wa Nairobi alitoa mitambo kumi ya kuhifadhia maiti kutumika kwenye hospitali hiyo.

Mara kadhaa, hospitali ya Pumwani imekuwa ikigonga vichwa vya habari kwa sababu mbaya: mwaka mmoja uliopita kulikuwa na madai ya biashara ya watoto, huku akinamama waliojifungua wakidai kuwa watoto wao hubadilishwa na kukabidhiwa wale waliokufa.

Inashukiwa wauguzi huwauza watoto hao kwa watu wengine, ambapo bei ya mtoto wa kiume ikisemekana kuwa shilingi 100,000 na wa kike kwa shilingi 50,000.

Kamati hiyo ya Seneti ilitarajiwa kuandaa ripoti na kuiwasilisha bungeni kujadiliwa.

Mwandishi: Shisia Wasilwa/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW