Usitishaji mapigano waanza kutekelezwa Gaza
19 Januari 2025Makubaliano ya kusitisha vita Ukanda wa Gaza,kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas,yameanza rasmi kutekelezwa Jumapili asubuhi, baada ya kucheleweshwa kwa masaa kadhaa.
Kuchelewa kwa hatua ya usitishaji vita kulitokana na mvutano uliozuka kuhusu orodha ya mateka wa mwanzo watakaoachiliwa chini ya mpango huo na kundi la Hamas.
Qatar ambayo ni mpatanishi kwenye makubaliano hayo imethitisha kwamba kundi la Hamas hatimae lilitowa orodha ya majina ya raia wa Israel watakaoachiliwa huru na kwamba sasa utekelezaji wa makubaliano hayo umekwishaanza rasmi.
Ofisi ya Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema kwamba hatua ya awali ya usitishaji mapigano kwa wiki sita itaanza kutekelezwa saa 11.15 asubuhi.
Mateka na wafungwa watakaoachiliwa
Kwa mujibu wa serikali ya Israel mateka watatu wa mwanzo wataachiliwa saa kumi jioni huku vyanzo nchini humo vikisema watakaoachiliwa ni wanawake watatu raia wa nchi hiyo.
Na katika muda huohuo awamu ya kwanza ya Wapalestina 90 waliofungwa katika jela za Israel wataachiliwa na kuchukuliwa na vikosi vya usalama kupelekwa Ukingo wa Magharibi au Gaza.
Japo haijakuwa wazi ikiwa muda huo ndio utakaozingatiwa au umebadilika kutokana na hatua ya kucheleweshwa utekelezaji makubaliano ya kusitisha vita.
Licha ya usitishaji huo mapigano kuwa na mwanzo uliokabiliwa na kizingiti,Wapalestina walionekana kusherehekea katika maeneo mbali mbali yaliyokabiliwa na vita vya muda mrefu huku maelfu yao wakionekana kuanza kurejea majumbani kwao.Soma pia: Viongozi wa dunia wapongeza makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza
Makubaliano hayo ni hatua ya kwanza kuelekea kumalizwa kabisa kwa vita katika eneo hilo na kuachiliwa kwa mateka takriban 100 waliotekwa nyara na kundi la Hamas katika uvamizi wao Israel,Oktoba 7 mwaka 2023, uliochochea vita vya Gaza.
Wakati huohuo waziri wa usalama wa wa Israel kutoka chama cha mrengo mkali wa kulia Itamar Ben-Gvir amejiuzulu nafasi yake, kama hatua ya kupinga kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Ben- Gvir ambaye chama chake kinashilikia viti sita bungeni atajiondowa kwenye serikali inayoongozwa na waziri mkuu Netanyahu na hatua hiyo huenda ikaiweka kwenye hali mbaya serikali ya Netanyahu.