1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Usitishaji vita waibua matumaini ya mateka zaidi kuachiwa

28 Novemba 2023

Makubaliano yaliyoafikiwa kati ya Israel na Hamas wiki iliyopita inatoa nafasi ya uwezekano wa kurefusha usitishaji mapigano ili kuachilia mateka 10 zaidi kila siku.

Israeli | Mateka wa Hamas waachiliwa huru
Eitan Yahalomi, 12, akitembea na mama yake kwenye kivuko cha mpaka cha Kerem Shalom, baada ya kuachiliwa kutoka Gaza ambako alishikwa mateka kufuatia shambulio la Oktoba 7 lililofanywa na kundi la wanamgambo wa Kipalestina Hamas, nchini IsraelPicha: Israel Defense Forces/REUTERS

Makubaliano ya kurefusha muda wa usitishaji mapigano kwa siku mbili yameibua matumaini ya urefushaji muda zaidi katika siku zijazo, hali ambayo itaruhusu pia misaada zaidi kupelekwa Gaza.

Israel na kundi la wanamgambo la Hamas wamekubaliana kurefusha muda wa kusimamisha mapigano hadi Jumatano, hali inayoleta matumaini ya uwezekano wa kuachiliwa huru mateka zaidi wanaoshikiliwa na Hamas na  Israel kuwaachilia wafungwa zaidi wa Kipalestina kutoka kwenye magereza yake.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameukaribisha urefushaji muda wa usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas.

Kupitia taarifa, von der Leyen ametoa wito tena "kwa magaidi wa Hamas kuwaachilia huru mateka wote waliowakamata kwenye shambulizi la kutisha la Oktoba 7.”

Hadi sasa zaidi ya mateka 50 wameachiliwa huru nayo Israel imewaachilia huru wafungwa 150 wa Kipalestina.Picha: Ibraheem Abu/REUTERS

Fahamu zaidi kuhusu: Mzozo wa Israel na Palestina

Kulingana na makubaliano hayo yaliyofikiwa wiki iliyopita, katika muda wa siku 10, jumla ya mateka 100 wanaweza kuachiliwa huru nayo Israel iwaachilie huru wafungwa 300 wa Kipalestina walioko katika magereza yake.

Hayo yakijiri, waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa kurudi tena Mashariki ya Kati wiki hii, mnamo wakati Marekani ikitarajia kwamba usitishaji mapigano utadumu kwa kuda mrefu ili kuruhusu mateka zaidi kuachiliwa huru.

Soma pia: Mapatano kati ya Israel na Hamas yaingia siku ya mwisho

Mateka waelezea mazingira mabaya walikoshikiliwa

Wanawake kumi na mmoja wa Israel pamoja na watoto walioachiliwa na Hamas, waliingia Israel usiku wa Jumatatu, ikiwa ni wiki saba tangu kundi la Hamas lilipowashika mateka na kuwapeleka Ukanda wa Gaza.

Ilikuwa awamu ya nne ya ubadilishanaji mateka kwa wafungwa wa Kipalestina katika siku ya nne ya makubaliano ya usitishaji mapigano kati ya vikosi vya Israel na Hamas, kundi ambalo Israel na Marekani miongoni mwa nchi nyingine zimeliorodhesha kuwa la kigaidi.

Makubaliano ya kusitisha vita Israel-Hamas kurefushwa?

02:12

This browser does not support the video element.

Mateka wa Israel walioachiliwa wameelezea hali mbaya ya maeneo walikokuwa wakishikiliwa na Hamas.

Mapema leo Jumanne, wafungwa 33 wa Palestina walioachiliwa na Israel waliwasili Jerusalem Mashariki, na mji wa Ukingo wa Magharibi wa Ramallah. Wafungwa hao walipokelewa kwa shangwe kubwa.

Soma pia: Mateka 13 wa Isarel na wengine 12 wa Thailand waachiwa na kuruhusiwa kuondoka kutoka kwenyae Ukanda wa Gaza

Japo pande mbili zimekubaliana kurefusha muda wa usitishaji mapambano, wachambuzi wanahofu kwamba ni suala la muda tu kabla ya vita kuanza tena.

Takriban mateka 240 walikamatwa na Hamas wakati wa shambulizi lake kusini mwa Israel Oktoba 7, ambapo pia takriban watu 1,200 waliuawa ndani ya Israel. Baada ya shambulizi hilo la kushtukiza, Israel ilitangaza vita dhidi ya Hamas. Kulingana na takwimu za wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 13,300 wameuawa tangu vita vilipoanza.

Vyanzo: APAE, DPAE