1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishaji wa mapigano Gaza uko njiani

20 Novemba 2012

Rais wa Misri Mohamed Mursi anategemea usitishaji wa mapigano huko Gaza unaweza ukafikiwa saa chache zijazo wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akitowa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo.

Rasi Mohammed Mursi wa Misri.
Rasi Mohammed Mursi wa Misri.Picha: Getty Images

Rais Mursi amesema mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza yatasitishwa leo hii Jumanne (20.11.2012) kwamba juhudi za kusitisha mapigano kati ya Wapalestina na Israel zitakuwa na matokeo mazuri katika kipindi cha masaa mchache yajayo. Mursi ametamka hayo baada ya kuhudhuria mazishi ya dada yake katika jimbo la kaskazini la al-Sharqiya nchini Misri.Afisa wa Hamas amesema mkuu wa kundi hilo Khalid Meshaal na wajumbe wake hivi sasa wako katika mkutano na mkuu wa ujasusi wa Misri anayesimamia mazungumzo ya kutafuta usuluhishi wa mzozo huo wa Gaza.Amesema kwamba sio siri wanakaribia kufikia makubaliano.Kwa mujibu wa afisa huyo Hamas ilikuwa bado inasisitiza kwamba Israel lazima iondowe vikwazo vyake vilivyodumu kwa miaka sita dhidi ya Ukanda wa Gaza ili kufikia makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Cairo kufuatia mazungumzo yake na Kiongozi wa Jumuiya ya Waarabu Nabil El Araby, Ban amesema anaunga mkono juhudi zinazoongozwa na Misri kukomesha mapigano kati ya Israel na makundi ya wanamgambo wa Israel katika Ukanda wa Gaza ulioko chini ya utawala wa Hamas.Ban amesema ujumbe wake uko wazi kwamba pande zote mbili lazima zisitishe mapigano mara moja na kwamba kuendelea kupamba moto kwa mzozo huo utaliweka eneo lote hilo katika hatari.Amesema mashaka ya usalama ya Israel ni ya halali na lazima yaheshimiwe kwa mujibu wa sheria ya kimataifa,lakini operesheni ya nchi kavu dhidi ya Gaza litakua jambo la hatari.Ban tayari ameondoka Misri na kulekea Jerusalem kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Viongozi wa Israel walipima faida na hasara za kutuma vikosi vyake na vifaru katika Ukanda wa Gaza unaokaliwa na idadi kubwa ya watu ikiwa ni miezi miwili kabla ya uchaguzi wa Israel na kudokeza kwamba wangependelea utatuzi wa kidiplomasia kwa mzozo huo jambo linaloungwa mkono na mataifa makubwa duniani akiwemo Rais Barack Obama wa Marekani,Umoja wa Ulaya na Urusi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- Moon akizungumza na waandishi wa habari mjini Cairo pembeni mwake ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Waarabu Nabil El Araby.Picha: Reuters

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ambaye yuko Mashariki ya Kati katika juhudi za kutuliza mzozo huo unaopamba moto amesisitza dhima kuu za usitishaji wa mapigano na usalama wa raia.Baada ya kukutana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Israel mjini Tel Aviv Avidor Lieberman, amesema lazima wajadili namna wanavyoweza kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano jambo ambalo ni muhimu kuliko kitu chochote kile.Westerwelle amesema Israel ni rafiki yao,Israel ni mshirika wao na ina kila haki ya kujilinda yenyewe na watu wake. Hata hivyo mwanadiplomasia huyo mkuu wa Ujerumani amesisitiza kwamba vifo zaidi vya raia lazima viepukwe.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akizungumza na waandishi wa habari mjini Tel Aviv.Picha: picture-alliance/dpa

Nayo Ikulu ya Marekani imesema kwamba waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Hilary Clinton anakwenda Mashariki ya Kati kwa mazungumzo mjini Jerusalem, Ramallah na Cairo kujaribu kuutuliza mzozo huo.Duru za Israel zinasema kwamba Clinton anatarajiwa kukutana na Netanyahu hapo Jumatano.Netanyahu na mawaziri wake waandamizi walijadili hatua zaidi za kuchukuwa katika mkutano uliomalizika alfajiri Jumanne.Afisa mwandamizi wa Israel amesema bila ya kutaka kutajwa jina lake baada ya kumalizika kwa mkutano huo kwamba kabla ya kupitisha uamuzi wa kuivamia Gaza waziri mkuu huyo wa Israel anakusudia kutumia juhudi zote za kidiplomasia kuona iwapo usitishaji wa mapigano utakodumu kwa muda mrefu unaweza kufikiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton.Picha: picture-alliance/dpa

Nao jumbe wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu wamewasili Gaza kwa kupitia mpaka wa Rafah nchini Misri.Afisa wa Hamas amesema ujumbe huo unajumuisha wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 10 zikiwemo Misri, Iraq,Morocco,Saudi Arabia, Sudan, Tunisia na Uturuki.Ujumbe huo unafanya ziara ya kuonyesha mshikamano na wananachi wa Gaza.Maroketi yanayorushwa na Wapalestina dhidi ya Israel na mashambulizi ya anga ya Israel yameendelea kwa siku ya saba mfululizo.Wanamgambo wa Hamas wamesema wamefyetuwa makombora 16 dhidi ya mji wa Beersheba ulioko kusini mwa Israel baada ya jeshi la Israel kushambulia takriban maeneo 100 huko Gaza wakati wa usiku yakiwemo maghala ya silaha na makao makuu ya Benki ya Waislamu yalioko huko Gaza.Takriban Wapalestina zaidi ya 110 wameuwawa katika mapigano hayo ya wiki moja wengi wao wakiwa ni raia wakiwemo watoto 27. Waisrael watatu waliuawawa wiki iliopita wakati kombora lililovurumishwa kutoka Gaza kuipiga nyumba yao.

Moshi ukifuka huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza kufuatia shambulio la Israel Jumanne(20.11.2012)Picha: Reuters

Mwandishi.Mohamed Dahman /RTRE/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW