1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishwaji mapigano Iran matatani

8 Mei 2026

Usitishwaji mapigano unaoyumba katika vita vya Iran umetiliwa doa zaidi Ijumaa baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu kujibu mashambulizi ya makombora na droni.

Meli ya mafuta ikiwa imetia nanga mlango bahari wa Hormuz
Meli ya mafuta ikiwa imetia nanga mlango bahari wa HormuzPicha: Amirhosein Khorgooi/ISNA/AP Photo/picture alliance

Haya yanafanyika saa chache baada ya Marekani kusema kuwa imezima mashambulizi katika meli tatu za jeshi la wanamaji katika Mlango Bahari wa Hormuz na kushambulia miundo mbinu ya kijeshi ya Iran.

Iran na Marekani wanashambuliana huku wapatanishiwakiwa wanatafuta makubaliano ya kusitisha mapigano, ila hadi sasa wamekwepa kurejea katika vita kamili.

Waziri Mkuu wa Pakistan alipokuwa akizungumza katika televisheni ya taifa nchini humo amesema Islamabad inasalia kwenye mazungumzo na Iran na Marekani kutwa kucha kuhakikisha kuwa vita vinasitishwa na muda wa kusitisha mapigano unarefushwa.

Tehran yachunguza mapendekezo ya Marekani

Kufikia sasa haijawa wazi bado pande hizo mbili ziko karibu kwa kiasi gani kukubaliana katika masuala kama mpango wa nyuklia wa Iran, ambao Marekani na Israel waliapa kuusambaratisha walipoanza vita mnamo Februari 28 au hata suala la Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu ambayo Iran imeifunga ili kuuwekea shinikizo uchumi wa dunia.

Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif akizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas AraghchiPicha: Pakistan's Prime Minister Office/AFP

Hapo Alhamis Tehran ilisema inayachunguza mapendekezo ya hivi karibuni ya kumaliza vita yaliyowasilishwa na Marekani kupitia Pakistan, ambaye ndiye mpatanishi. Lakini Rais Donald Trump alipuuza makabiliano yaliyotokea kati ya Iran na jeshi la wanamaji la Marekani akisema usi´tishwaji mapigano bado ungalipo.

Trump lakini amerudia kitisho cha kuishambulia Iran kwa mabomu iwapo haitokubali mkataba utakaotoa nafasi ya usafirishaji wa mafuta na gesi ambao umesitishwa na mzozo huo.

"Ndio mapigano yamesitishwa. Wametujaribu leo, ila tukawashambulia. Nitawafahamisha iwapo usitishwaji mapigano utavunjika...hautohitaji kujua kama mkataba wa kusitisha mapigano umevunjwa, hautohitaji kuambiwa. Utaona tu mwanga mkubwa unatokea Iran. na bora wasaini makubaliano tuliyowasilisha kwa haraka," alisema Trump.

Wakati huo huo, China kupitia wizara yake ya mambo ya kigeni imethibitisha kuwa meli yake inayosafirisha bidhaa za mafuta imeshambuliwa katika Mlango Bahari wa Hormuz, na kuelezea hofu yake kwa meli zinazoshambuliwa katika mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China Lin Jian, amesema, meli hiyo ilikuwa na raia wa China ila hakuna aliyeuwawa katika mashambulizi hayo.

Meli 1,500 zimekwama Mlango Bahari wa Hormuz

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya bahari karibu meli 1,500 na wafanyakazi 20,000 bado wamekwama Ghuba kutokana na vizuizi vya Iran katika Mlango Bahari wa Hormuz.

Baadhi ya meli zilizokwama Mlango Bahari wa HormuzPicha: Amirhosein Khorgooi/ISNA/dpa/picture alliance

Kwengineko huko Mashariki ya Kati afisa mmoja wa Marekani amesema Lebanon na Israel watafanya awamu nyengine ya mazungumzo wiki ijayo kati ya tarehe 14 na 15 mjini Washington, licha ya shambulizi jipya la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alidai kuwa Israel ilihusika na mauaji ya kamanda mkuu wa Hezbollah akidai hakuna ""gaidi" atakayekoswa na mashambulizi ya Israel.

Vyanzo:Reuters/AFPE/AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW