1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uswisi imekubali kuwa mpatanishi katika mazungumzo Cameroon

18 Julai 2019

Taifa la Uswisi limekubali kuwa mpatanishi katika mazungumzo kati ya serikali ya Cameroon na viongozi wa makundi yanayotaka kujitenga katika kutafuta suluhu ya amani kumaliza mgogoro unaoendelea kwa mwaka wa tatu

Kamerun Polizisten in Buea
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mgogoro huo umeisakama Cameroon hasa katika mikoa ambayo inatumia lugha ya Kiingereza ya Kazkazini Magharibi na Kusini Magharibi tangu mwaka 2016. Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema kwamba sababu za mgogoro huo zitapata ufumbuzi iwapo tu vikao hivyo vya upatanishi vitajumuisha maoni mbali mbali kutoka kwa wanaozungumza kiingereza nchini Cameroon.

Kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Nkongho Felix Agbor Balla, Uswisi inapaswa kuhakikisha inawahusisha watu mbali mbali sio tu wale wanaoshiriki katika vita vinavyoendelea, lakini pia kuzialika taasisi mbali mbali kama Umoja wa Afrika pamoja na serikali ya Canada kutokana na mahusinao ya muda mrefu ya taifa hilo na Cameroon.

Wazazi wakisubiri taarifa za watoto wao katika shule ambapo wanafunzi 79 walitekwa nyara Bameda, CameroonPicha: Reuters/B. Eyong

Mapigano nchini Cameroon ndio mgogoro mkubwa ambao umepuuzwa na jamii ya kimataifa licha ya kuwa na maafa makubwa yanayosababishwa na jeshi na makundi ya wanaotaka kujitenga. Jeshi limehusika na uhalifu dhidi ya binadamu kwa wananchi walioko katika mikoa inayotumia lugha ya kiingereza, haya ni kulingana na kituo cha haki za binadamu na demokrasia Afrika, tawi la Cameroon pamoja na kituo cha haki za binadamu cha Raoul Wallenberg kilichoko nchini Canada.

Mzozo katika taifa hilo ulianza mwaka 2016 kama ombi rahisi tu la Mawakili na Walimu wa Kiingereza walipofanya maandamano ya amani kudai haki za kimsingi na kisiasa baada ya muda mrefu wa kutengwa na serikali ambayo inahodhiwa na wengi wanaotumia lugha ya kifaransa. Mawakili na Waalimu hao walitaka kuajiriwa kwa mahakimu na walimu wanaozungumza lugha ya kiingereza katika Mahakama na Shule zinazotumia Kiingereza.

Wanajeshi wakiwa na bunduki wakishika doria katika mikoa ya wanaozungumza KiingerezaPicha: DW/F. Muvunyi

Ni kutokana na hilo ambapo maandamano hayo yalibadilika na kuwa mgogoro mkubwa katika mikoa inayotumia kiingereza, watu waliokuwa na maoni tofauti waliuliwa na watu waliokuwa na misimamo mikali ya kutaka kujitenga na taifa la Cameroon. Kauli za chuki zilienea katika vyombo vya habari na katika majadiliano ya serikali kwa kiwango cha kutisha jambo ambalo Nkongho Felix alisema kulingana na historia jambo hilo linaweza kusababisha hasara kubwa na mauaji ya halaiki.

Vijiji vinatiwa moto na Wanajeshi

Wanajeshi wamekuwa na mbinu ya kuvitia moto vijiji mara kwa mara huku wakiwaua wananchi kwa kuwapiga risasi na wakati mwengine wakiwaacha maiti kando kando mwa barabara. Zaidi ya vijiji 200 vimetiwa moto huku mashambulizi yakiendelea kuzidi. Matokeo yake ni watu kuchomwa wakiwa hai ndani ya nyumba zao. Mzee wa miaka 70 aliyekuwa masito aliteketea baada ya kushindwa kuwasikia majirani waliokuwa wakitoa tahadhari ya moto.

Waandishi wa habari wanaoangazia mzozo huo wamekuwa wakishikwa na kupigwa na hata kutiwa kizuizini bila ya kuandikiwa mashtaka wala kuruhusiwa kuonana na mawakili. Visa vya unyanyasaji wa kijinsia hasa vinavyolenga wasichana walio na umri chini ya miaka 18 vimeongezeka. Kwa sasa taifa la Cameroon ni nambari sita miongoni mwa mataifa yaliyo na idadi kubwa ya watu walioyakimbia makaazi yao Ulimwenguni. Kiasi cha watu laki tano wanaishi mwituni bila ya maji na chakula chakutosha na vile vile kukosa ulinzi.

Katika mikoa inayozungumza kiingereza pekee, kiasi cha Wakameruni milioni moja na laki tatu wanahitaji kwa dharura misaada ya kiutu

(DW)