Utafiti: Migogoro ya kivita yauwa watoto milioni 5 Afrika
31 Agosti 2018Utafiti mpya uliochapishwa kwenye jarida la masuala ya afya la The Lancet umeonesha kuwa migogoro katika mataifa kama vile Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imechangia vifo vya hadi watoto milioni tano wenye wenye umri wa chini ya miaka mitano kati ya mwaka 1995 na 2015.
Idadi hiyo inajumlisha waathirika miliotni tatu wenye umri wa mwaka mmoja wa chini, na ni ya juu zaidi kuliko ilivyokadiriwa, huku wanasayansi wakisema vifo vya kiraia vya watoto vimezidi vile vilivyotokana na migogoro ya kivita kwa zaidi ya vitatu kwa moja.
Athari za vita
Mkuu wa watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Stanford Marekani, Eran Bendavid, anasema athari za vita zinazaa misururu ya athari nyingine zisizo za moja kwa moja kwa jamii, ambazo zinasababishwa na magonjwa ya kuambukizwa, utapiamlo, na kuvurugwa kwa huduma za msingi kama vile maji, usafi wa mazingira na huduma za uzazi.
Utafiti huo ulizingatia migogoro karibu elfu 15,500 katika mataifa 34 miongoni mwa mataifa 54 katika muda wa miongo miwili, vile vile kutathmini data kuhusu vifo vilivyotokana na migogoro ya kivita, pamoja na watoto waliozaliwa wakiwa hai na waliofariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Watoto walioko katika hatari kubwa
Ilibainika kwamba watoto waliozaliwa katika maeneo yaliyo kilomita 50 kutoka maeneo yanayoshuhudia vita, walikuwa katika hatari kubwa ya kufariki dunia, asilimia 8 katika mwaka wao wa kwanza, wakilinganishwa na wanaozaliwa katika eneo hilo miaka ambayo hakushuhudiwi vita.
Watafiti wanasema athari za vifo vya watoto ziliongezeka hadi asilimia 30 wakati vita vilikuwa vibaya zaidi, na kuongeza kuwa viwango vya watoto wanaozaliwa wakiwa wamefariki viliongezeka mara nne zaidi, vita viliposhuhudiwa kwa miaka mitano au zaidi.
Athari za kuongezeka kwa vifo vya watoto ziliendelea hadi katika maeneo yaliyo umbali wa kilomita 100 kutoka maeneo yaliyoshuhudia migogoro, na athari kwa watoto waliozaliwa miaka minane baada ya vita hivyo zilipungua.
Watoto hao walichangia takriban asilimia 7 ya vifo, ambayo ni mara 20 zaidi ya asilimia 0.4 iliyokadiriwa awali katika ripoti ya Dunia kuhusu mzigo wa magonjwa ya mwaka 2015.
Umuhimu wa kutambua ukubwa wa tatizo
Msemaji wa Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu eneo la Afrika Mashariki Crystal Wells amesema, "watoto ndio wanaoathirika na utapiamlo na magonjwa yanayoweza kuzuilika, ambayo yanakuwa na athari kubwa wakati familia zinapokoseshwa makaazi na kulazimika kuishi kwa chakula kidogo na maji salama ya kunywa."
Wafanyakazi wa misaada katika hospitali na vituo vya matibabu kwenye maeneo ya vita, wamesema kwamba wahudumu pamoja na vituo vya matibabu vimelindwa chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, na makundi ya wapiganaji yanapaswa kuzingatia sheria hiyo.
Watafiti hao wameeleza matumaini kwamba utafiti huu utatoa shinikizo kuhusu ukubwa wa athari za vita kwa watoto, na umuhimu wa uingiliaji kuhakikisha masuala ya afya ya watoto wanaoishi katika maeneo ya vita yanashughulikiwa ipasavyo.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/RTRE
Mhariri: Iddi Sessanga