Wananchi wengi waridhika na huduma za mahakama Zanzibar
10 Machi 2026
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mijadala mikali kuhusu utendaji wa mahakama Zanzibar, hasa katika suala la utoaji wa haki. Baadhi ya wananchi wamekuwa wakieleza kupoteza imani na taasisi hiyo, huku wengine wakitaka maboresho zaidi katika mfumo wa haki.
Hata hivyo, utafiti uliofanywa mwaka jana na taasisi ya utafiti ya REPOA unaonyesha kuwa wananchi wengi bado wanaridhika na huduma zinazotolewa na mahakama Zanzibar.
Matokeo ya utafiti huo yamezua mjadala mpya, hasa baada ya malalamiko yaliyotolewa hivi karibuni kuhusu uhuru wa mahakama katika kushughulikia mashauri ya uchaguzi.
Baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, chama cha ACT Wazalendo kiliwasilisha kesi kadhaa kupinga matokeo ya ubunge na uwakilishi. Baadhi ya wananchi wanaamini kuwa haki haikutendeka kikamilifu katika baadhi ya mashauri hayo.
Mmoja wa wananchi, Mustafa Sharif, alisema licha ya matokeo ya utafiti huo, bado ana mashaka kuhusu utoaji wa haki.
"Kwa upande wangu nasikitika kuona kwamba mahakama zetu hazipo katika kutoa haki ipasavyo. Hii imejidhihirisha katika kesi za uchaguzi wa Oktoba 2025 ambapo kwa maoni yangu haki haikupatikana. Uwajibikaji na uwazi haukuchukua nafasi yake,” alisema.
Naye mwananchi mwingine, Makiyye, anaamini bado kuna haja ya mahakama kufanya juhudi zaidi ili kuimarisha imani ya wananchi.
"Matokeo ya utafiti huu hayaondoi haja ya mahakama kufanya kazi ya ziada katika utoaji wa haki kwa makundi mbalimbali ya wananchi. Inawezekana watu wana imani na mifumo ya mahakama, lakini bado kuna kazi ya kufanya ili kujenga imani thabiti ya wananchi,” alisema.
Utafiti ulivyofanyika
Utafiti huo wa REPOA ulifanyika katika mahakama zote za Zanzibar, kuanzia Mahakama Kuu hadi mahakama za mwanzo katika wilaya zote za Unguja na Pemba.
Watafiti waliwahoji makundi mawili ya watu: watumiaji wa mahakama wenye mashauri mahakamani, wananchi ambao hawana kesi lakini wanafahamu huduma za mahakama.
Hakimu wa Mkoa na pia Mratibu Msaidizi wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama, Khamis Ali Simai, alisema utafiti huo ulifanywa na taasisi huru ili kuhakikisha matokeo yake yanaaminika.
"Utafiti huu umefanywa na kampuni ya REPOA, taasisi kubwa ya utafiti nchini Tanzania. Tuliamua kuchagua taasisi huru ili kuhakikisha matokeo yake hayana upendeleo na yanaonyesha hali halisi ya huduma za mahakama,” alisema Simai.
Katika utafiti huo, watafiti walitumia vigezo vitano kupima ubora wa huduma za mahakama. Vigezo hivyo ni: kiwango cha kuridhika kwa wananchi; urahisi wa kupata huduma; ufanisi wa utoaji wa huduma; uwazi katika utendaji wa mahakama na; ubora wa huduma zinazotolewa.
Simai alieleza kuwa watafiti walizungumza na watumiaji wa mahakama waliokuwepo mahakamani wakati wa utafiti pamoja na wananchi kutoka maeneo ya karibu na mahakama. Makundi hayo yalijumuisha wafanyabiashara, mawakili pamoja na wananchi wa kawaida.
Uelewa mdogo wa mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro
Pamoja na matokeo chanya kwa ujumla, utafiti huo pia umebaini changamoto katika uelewa wa wananchi kuhusu mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro.
Kwa mujibu wa utafiti huo, ni asilimia 17 tu ya wananchi wanaofahamu uwepo wa mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro (Alternative Dispute Resolution – ADR), ambazo zinaweza kutumika kusuluhisha migogoro bila kufungua kesi mahakamani.
Kwa ujumla, matokeo ya utafiti yanaonyesha kiwango kikubwa cha kuridhika kwa wananchi kuhusu huduma za mahakama Zanzibar.
Takribani asilimia 80 ya wananchi waliohojiwa walisema wanaridhika na huduma za mahakama. Asilimia 70 walisema huduma hizo zinapatikana kwa urahisi. Asilimia 67 waliona kuna uwazi katika utoaji wa huduma. Asilimia 65 walisema ubora wa huduma zinazotolewa unaridhisha.
Licha ya takwimu hizi, wachambuzi wanasema mahakama bado zinahitaji kuendelea kuboresha uwazi, uwajibikaji na mawasiliano na wananchi ili kuimarisha zaidi imani ya umma katika mfumo wa haki Zanzibar.