Utafiti wabaini ongezeko la mashambulizi kwa watoa misaada
17 Agosti 2020Utafiti huo aidha umeeleza kuwa wafanyakazi wa afya ndio wahanga wakuuu wa mashambulizi hayo. Katika utafiti huo uliotolewa Jumatatu na shirika la kimataifa lenye kufuatilia masuala ya kibinadamu "Humanitarian Outcomes'', mnamo mwaka uliopita wa 2019 mashambulizi makubwa yapatao 277 yalifanyika dhidi ya wafanyakazi wa kutoa misaada katika mataifa yanayokabiliwa na machafuko.
Kwa mjuibu wa utafiti huo, jumla ya watoa misaada 483 waliuuliwa, kutekwa nyara au kujeruhiwa mnamo mwaka huo, hiyo ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kutokea tangu shirika hilo kuanza kurekodi visa hivyo mnamo mwaka 1997.
Akizungumzia kuhusu utafiti huo, Mkuu wa shirika la Kimataifa la Norway la kutoa misaada kwa wakimbizi, Jan Egeland ameonesha wasi wasi juu ya kuongezeka kwa mauaji ya wafanyakazi wa misaada.
Wahudumu wanatakiwa kulindwa
Aidha ametaka wahudumu hao kupewa ulinzi thabiti huku akieleza kuwa kama hilo halitafanyika huenda watu wengi katika mataifa yenye mizozo wakaachwa bila misaada ya kiutu.
Wakati huo huo, uchambuzi wa ripoti kuhusu Usalama wa Wahudumu wa Afya ambayo inatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwezi huu unaeleza kuwa zaidi ya 40% ya idadi ya waliouuliwa ni wafanyakazi wa afya. Idadi hiyo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na miaka iliopita.
Kulingana na ripoti hiyo, wafanyakazi wa afya wamekuwa wakilengwa hususani nchini Syria, nchi ambayo imetajwa kuwa hatari zaidi kwa wahudumu wa kutoa misaada. Mnamo mwaka uliopita visa 47 vilirekodiwa dhidi ya watoa misaada huku 36 wakipoteza maisha yao.
Nako nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, shirika la "Humanitarian Outcomes” limebaini kuwa mnamo mwaka jana zaidi ya wahudumu wa afya 27, ambao walikuwa wakiwatibu wagonjwa wa Ebola nchini humo walishambuliwa. Ongezeko hilo ni kubwa zaidi kuwahi kutokea
(Reuters)