1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti waonyesha umaarufu wa Kansela Merkel umeporomoka

5 Agosti 2016

Utafiti mpya wa maoni ya watu nchini Ujerumani, unaonyesha kuwa Kansela Angela Merkel amepoteza uungwaji mkono kwa kiwango kikubwa, kufuatia mashambulizi kadhaa yaliyotokea nchini humo hivi karibuni.

Kansela Angela Merkel (kushoto) na Horst Seehofer
Kansela Angela Merkel (kushoto) na Horst SeehoferPicha: Getty Images/S. Gallup

Kulingana na ripoti ya utafiti huo ujulikanao kama DeutsclandTrend Survey, uungwaji mkono wa Kansela Angela Merkel umefika katika kiwango cha chini kabisa katika kipindi cha miezi sita iliyopita. Utafiti mwingine ulipofanywa mwezi Julai, asilimia ya 57 ya watu waliohojiwa walikuwa wakimuunga mkono kiongozi huyo, lakini utafiti wa hivi karibuni kabisa umeonyesha kuwa ni asilimia 47 tu wanaosalia naye.

Utafiti huo ulifanya baada ya mfululizo wa mashambulizi ambayo hayana uhusiano, yaliyofanywa na watu ambao kwa nyakati tofauti walikuwa wameomba hifadhi nchini Ujerumani.

Kansela Merkel ameitetea sera yake kuhusu wakimbizi, akizungumza katika mkutano wa kila mwaka na waandishi wa habari wiki iliyopita. Bi Merkel alisisitiza uamuzi wake wa kuwaruhusu mamia ya wakimbizi kuingia nchini Ujerumani kuanzia majira ya kiangazi mwaka jana, ulikuwa sahihi.

Wengi hawaridhiki

Asilimia 65 ya watu waliohojiwa katika utafiti huo wa maoni, walisema hawaridhishwa na sera hiyo ya Kansela Merkel. Hata hivyo, utafiti huo haukuwapa watu fursa ya kueleza sababu zao za kutoridhika. Asilimia 34 ya waliohojiwa walisema wanaamini nchi yao iko katika mkondo mzuri kuhusiana na sera hiyo kuhusu wakimbizi, hiyo ikiwa asilimia ndogo kabisa tangu majira ya mapukutiko.

Mashada ya maua mahali palipofanyika mashambulizi na mauaji mjini MunichPicha: DW/D. Regev

Hali nyingine iliyodhihirika katika utafiti huo wa maoni, ni kuongezeka kwa uungwaji mkono kwa Horst Seehofer, Waziri Mkuu wa Jimbo la Bavaria, na mkuu wa CSU, chama ndugu na CDU cha Kansela Angela Merkel. Seehofer ambaye alizipinga sera za Kansela Merkel kuhusu hifadhi kwa wakimbizi, sasa anaungwa mkono na asilimia 44, hilo likiwa ongezeko la asilimia 11.

Asilimia 64 ya walioulizwa walisema wanaamini wanasiasa wa CSU cha Horst Seehofer wanajitahidi kufanya kazi kwa maslahi ya chama, kuliko kwa malengo ya mafanikio ya serikal.

Bado CDU/CSU wanayo nafasi

Kwa hali jumla, muungano wa CDU/CSU bado unaongoza kwa kupendelewa na asilimia 34 ya watu, wakati chama cha SPD ambacho pia kimo katika serikali ya mseto, kikiungwa mkono na asilimia 22.

Picha: Getty Images/J. Koch

Vyama vingine ambavyo kulingana na utafiti huu mpya wa maoni vinao uungwaji mkono wa maana ni pamoja na chama cha walinzi wa mazingira, Greens ambacho kinaungwa mkono na asilimia 13, na kile kinachofuata sera za mrengo wa kushoto, Die Linke, ambacho uungwaji mkono wako ni asilimia 9.

Chama chenye mrengo mkali wa kizalendo cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD kinaungwa mkono na asilimia 12 ya waliofanyiwa utafiti, huku kile kinachopendelea biashara huria cha Free Democrats, kikiambulia asilimia tano.

Mnamo mwezi Februari mwaka huu umaarufu wa Kansela Angela Merkel ulishuka kabisa hadi asilimia 46, lakini, katika kile kinachotazamwa kama tabia ya kubadilikabadilika kwa maoni ya wapiga kura wa Ujerumani, umaarufu huo ulipanda tena na hata kufika kiwango cha juu, hata baada ya Uingereza kupiga kura kujiondoa katika Umoja wa Ulaya mwezi Juni, na jaribio la mapinduzi lililofeli nchini Uturuki mwezi uliopita wa Julai.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afp, dpa

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW