1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utamaduni

Zanzibar: Utamaduni na historia tajiri ya mikate

13 Oktoba 2025

Zanzibar ina haiba ya kipekee kutokana na jamii yake yenye mchanganyiko wa watu kutoka mataifa mbalimbali, kwani kila kundi likibeba mila, desturi na mapishi yao.

Zanzibar, Tanzania 2025 | Mikate ya Zanzibar
Mkate wa Kara unaotumiwa na jamii ya Wahindi na WabohoraPicha: Salma Said/DW

Mchanganyiko huu umeifanya Zanzibar kuwa na utajiri mkubwa wa vyakula, tofauti na sehemu nyingi nyingine ambako aina za vyakula ni chache. Hii inaonyesha jinsi Zanzibar inavyoainisha safari yake ya mikate, ladha, historia na asili zake.

Utajiri wa vyakula vya Zanzibar unaonekana hata katika mapishi. Wakati katika nchi nyingi mapishi ya mchele ni mawili au matatu, Zanzibar kuna zaidi ya 20, huku wali pekee ukiwa na zaidi ya mapishi 10, ikwemo ule wa asumini!

Na ukigeukia mikate, ndipo utajua ladha ya Zanzibar haina kifani. Zipo aina nyingi za mikate kutoka mataifa tofauti zikitokana na watu waliotoka Ghuba ya Uajemi, Iran, Pakistan, Uturuki na Syria. Lakini kwa Zanzibar, athari kubwa zaidi ni kutoka Oman, India na visiwa vya Comoro. Wazee wa visiwa hivi wanasema kuna zaidi ya aina 100 za mikate, ingawa hakuna maandiko rasmi yanayothibitisha hilo.

Histora ndefu ya mikate ya Zanzibar  

Miongoni mwa wanaojua historia yake ni Farid Hamid, mtunzaji wa kumbukumbu za mambo ya kale, ambaye anasema Mikate ina historia ndefu sana Zanzibar na kwamba mikate ya visiwani hivyo ni kama utamaduni mkubwa uliobeba sura ya Wazanzibari.

''Tangu zamani watu walipokuja kwa jahazi, kila mmoja alileta mikate yao. Waarabu, Wahindi, Wabantu na hata Wazungu. Unguja mikate ni mingi sana. Zamani watu walikuwa wakioka, lakini Wazungu walipokuja wakaanzisha maeneo ya kuokea mikate. Wahindi nao wakaja na yao, na Waswahili wakachanganya na utamaduni wao,'' alisema Hamid.

Miongoni mwa mikate maarufu visiwani Zanzibar ni mkate wa mofa, ajemi, chila, ufuta, mkate wa sinia, mkate wa Kara, mkate wa mchele, mkate wa mayai wenye zabibu, mkate wa bwana na mingine mingi zaidi.

Akizungumza na DW Kiswahili, Hamid anafafanua kuwa Waswahili walikuwa na desturi ya kunywa chai na mikate. Wahindi walipoingia Zanzibar, walipeleka mkate wa ufuta au mkate wa mayai, na siku hizi, mkate wa sinia nao umekuwa maarufu sana. Kwa mujibu wa mtunzaji huyo wa kumbukumbu za mambo ya kale, watu waliokwenda Zanzibar kila mmoja alipeleka mkate wake.

Mikate ya UfutaPicha: Salma Said/DW

Makabila yenye asili ya Kihindi yana aina nyingi zaidi za mikate, na hata namna ya kutengeneza hutofautiana kama iliyozoeleka kwa Waswahili. Mikate hiyo hutumia unga wa ngano wa rangi ya udongo, lakini pia unga mweupe, na huokwa juu ya chungu au gae la udongo.

Abdulatif Sanya Jussa, anasema kwa jamii za Kihindi, mikate yao huwa inakaangwa zaidi kuliko kuchomwa. ''Sisi tuna mikate tunaita parata na chapati, tunaioka juu ya chuma au gae la udongo, kwa kutumia unga wa mtama au mawele. Pia tuna mkate wa naan, unaochomwa kwa mafuta, unaotiwa rangi ya njano, mayai na sukari kidogo. Huo ni mkate unaopendwa sana,'' alibainisha Jussa.

Mikate hutumika hata kwa mlo wa mchana na jioni

Aina nyingi za mikate iwe ya kuchoma, kukaanga au kupambwa, ni sehemu muhimu ya kifungua kinywa cha Wazanzibari. Lakini siku hizi, mikate hiyo imevuka mipaka ya asubuhi na hutumika pia katika mlo wa mchana na hata usiku.

Miongoni mwa wanawake wanaotunza ladha ya mikate ya asili ni Abla Sultan, mwenye asili ya visiwa vya Comoro. ''Mikate ya kwetu Ngazija ni kama ya hapa Zanzibar, isipokuwa moja mkate wa Kingazija au Gudibudi. Mikate mingine kama chila na mkate wa sinia yote tunaoka, lakini Gudibudi ni ya kwetu peke yetu, hauokwi popote isipokuwa Ngazija,'' alisema Abla.

Wakaazi wa Zanzibar wamejenga utamaduni wa kula mikate mbalimbali kila asubuhi kama sehemu ya maisha yao. Na pale wanapokosa mikate ya asili, boflo kutoka kwenye maeneo ya kuoka mikate huwa mbadala wa haraka. Mikate mipya, ya moto, yenye harufu tamu inayokamilisha asubuhi ya Kizanzibari.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW