1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utapiamlo waikumba Ethiopia

Anaclet Rwegayura14 Julai 2005

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na maendeleo ya watoto, UNICEF, limetahadharisha kuwa watoto wapatao 170,000 huenda wakafa mwaka huu nchini Ethiopia kutokana na utapiamlo ambao umeikumba sehemu kubwa ya nchi hiyo.

Shirika la UNICEF linaomba msaada wa haraka kuwasaidia watoto wa Ethiopia
Shirika la UNICEF linaomba msaada wa haraka kuwasaidia watoto wa EthiopiaPicha: UNO
Katika taarifa yake kwa wahisani, UNICEF imesema kuwa inahitaji dola 42 milioni kuepusha janga hilo. Wakati huu watoto 6,800,000 wanahitaji kufanyiwa mpango wa dharura wa lishe, kuondoa minyoo matumboni na kupewa kinga dhidi ya surua.

Hali kadhalika watu wasiopungua 1,200,000 nchini Ethiopia wanahitaji msaada wa dharura wa maji safi na huduma nyingine za kuepusha magonjwa yatokanayo na uchafu.

"Hali ya utapiamlo mkali kwa watoto wa Ethiopia imefikia kiwango cha kutosha," amesema Mwakilishi wa UNICEF nchini, Bwana Bjorn Ljungqvist. Kiwango cha tatizo hili kimethibitishwa na kaguzi za lishe zilizofanywa kwa mpango unaodhaminiwa na UNICEF.

Hali ya kutisha ya utapiamlo imekutwa katika kambi za wakimbizi za Fugnido na Bonga zilizo katika mkoa wa Gambella magharibi mwa Ethiopia.

Ukaguzi uliofanywa na Mpango wa Chakula Duniani pamoja na Shirika Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi umeonyesha kiwango cha juu kabisa cha utapiamlo kwa asilimia 29 katika kambi hizo.

Hali kama hiyo pia imekutwa katika eneo la Fik katika Mkoa wa Somali ulioko mashariki mwa Ethiopia. Jirani na mkoa huo, wataalam wa lishe wanaofanya kazi katika Mkoa wa Kusini na Mkoa wa Oromiya wameripoti ongezeko la watu ambao wamedhoofu kutokana na ukosefu wa lishe.

Uchambuzi wa takwimu zilizopo wakati huu unaonyesha kuwa wako watoto 136,000 ambao wanakabiliwa na hali mbaya sana ya utapiamlo nchini Ethiopia, na wengine 360,000 wako hatarini kufikia hali hiyo.

Shirika la UNICEF limeonya kuwa vifo vya watoto huenda vikatokea kwa kasi ikiwa hazikuchukuliwa hatua za haraka kutoa matibabu au kinga dhidi ya surua, malaria, maradhi ya kuhara na ugonjwa wa pafu.

UNICEF imeeleza kuwa hali hii imezidi kuwa mbaya kutokana na mvua haba iliyonyesha katika maeneo yenye mifugo mingi ukanda wa mashariki mwa Ethiopia mwaka jana pamoja na ukame uliokumba maeneo hayo miaka miwili nyuma.

Tangu mapema mwaka huu familia nyingi za wafugaji hawakuwa na chakula cha kutosha ambapo ukame umesababisha vifo vya mifugo yao mingi.

Kuhusu huduma ya maji, UNICEF bado inakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha kuweza kufikisha maji safi kwa watu wenye shida. Kati ya dola 15 milioni ambazo shirika hilo linahitaji kutekeleza mpango wa dharura wa maji tangu mwanzo wa mwaka huu, zimepatikana dola 2,700,000 tu.

Hapo awali UNICEF ilitegemea kutoka huduma ya maji kwa kutumia magari ya matanki ikiwa na lengo la kuwafikia watu 420,000. Lakini mpaka wakati huu huduma hiyo imefikia theluthi moja ya walengwa katika mikoa ya Afar na Somali.

Kwa miezi mitatu ijayo, UNICEF inahitaji dola 2,000,000 kwa ajili ya kusambaza maji na huduma za usafi katika vituo ambavyo vimeathirika zaidi, hasa mahali ambapo lishe inatolewa kwa watoto waliodhoofika.

Mara kwa mara Ethiopia hukumbwa na majanga ya ukame, mafuriko na maradhi ambayo kila mwaka husababisha wananchi wake wengi kutegemea misaada ya wahisani ili waishi.

Majanga hayo yakichanganyikana na umasikini unaowakabili watu wengi, husababisha ombaomba wengi, watoto na watu wakubwa, kukimbilia mijini hasa Addis Ababa ambako hata hivyo hawapati nafuu yoyote.
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW