1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utata katika ziara ya Macron

2 Machi 2023

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, anatarajiwa kuwasili mjini Kinshasa Jumamosi ijayo, ikiwa kituo cha mwisho cha ziara yake ya Afrika inayoanza Alhamis nchini Gabon.

Frankreich Präsident Macron
Picha: STEPHANE MAHE/AFP

Ziara hiyo Inajiri huku Wakongo wakiishutumu Ufaransa kwa kuiunga mkono Rwanda, wanayodai inawaunga mkono waasi wa M23 ambao Kinshasa inawataja kuwa magaidi wanaovuruga usalama mkoani  Kivu Kaskazini.

Kuelekea ziara ya Rais Emmanuel Macron nchini Kongo, Wakongo wamegawanyika kuhusu ujio wa rais huyo wa Ufaransa hapa Kinshasa. Christophe Mboso, Spika wa Bunge la Kitaifa alitoa wito kwa wanainchi kumkaribisha kwa furaha Rais Macron.

"Nilifuatilia mazungumzo baina ya Rais Macron na waandishi wa habari. Alitetea uhuru wa Kongo na kuomba mara kadhaa Rwanda iondoe wanajeshi wake na wasaidizi wao wa M23. Rais Macron anakuja, naomba watu wa Kongo kumkaribisha," alisema Mboso.

Macron afafanue msimamo wake kati ya Kongo na Rwanda

Akisindikizwa na ujumbe mkubwa, Rais Macron anatarajiwa kukutana na mwenzake wa Kongo Félix Tshisekedi, Profesa Jean-Jacques Muyembe ambaye ni Mkurugenzi  wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Tiba ya Viumbe (INRB) ambayo pia amepanga kuizuru.

Lakini kabla ya kuanza lolote, rais Emmanuel Macron ametakiwa kwanza kufafanua msimamo wake kuhusu mzozo baina ya Kongo na Rwanda, kama alivyoeleza Patrick Muyaya, msemaji wa serikali ya Kongo.

Jeshi la EACRF na wanamgambo wa M23 huko KibumbaPicha: GLODY MURHABAZI/AFP/Getty Images

"Kile ambacho Wakongo wanatarajia kutoka Ufaransa ni kujitolea wazi, kulaani Rwanda na kuchukua hatua dhidi yake ili kukomesha mashambulizi yake dhidi ya Kongo. Tupo wazi. Kabla ya kushughulikia masuala ya maendeleo, tunataka Ufaransa ifafanue msimamo wake kwa maneno ya wazi. Hatutaki hotuba za kutatanisha bali dhamira ya wazi ili  amani kurejea Mashariki," alisema Muyaya.

Wakongo wengi hawairidhii ziara ya Macron

Ukweli ni kwamba idadi kubwa ya Wakongo haijaridhia ziara ya Rais Macron.Kulikuwa na maandamano dhidi ya ziara hiyo    jana Jumatano mbele ya Ubalozi wa Ufaransa. Maandamano yaliyoandaliwa na kundi la harakati za kiraia. Jack Sinzahera kutoka shirika la harakati la Amka Kongo ni mmoja wa waandaaji.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix TshisekediPicha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

"Hatuwezi kumpokea nchini mwetu bwana Macron sababu Ufaransa kuwa nyuma ya mauwaji ya ndugu zetu mashariki na uporaji wa mali ya raia na waasi wa M23 mahali pote ambapo wanadhibiti. Bwana Macron ndiye anaunga mkono jeshi la Rwanda ambalo linaunga pia mkono M23," alisema Sinzahera.

Ni baada ya Brazzaville, mji mkuu wa nchi jirani ya Kongo, ndipo Emmanuel Macron atawasili Jumamosi mjini Kinshasa ambapo atakaa hadi Jumapili.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW