1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utata wazidi kuhusiana na mauaji ya wanafunzi

Charles Mwebeya17 Aprili 2007

Lawama zaidi zimeendelea kutolewa kwa uongozi wa chuo cha ufundi cha Virginia nchini Marekani kwa kushindwa kutoa taarifa mapema kwa wahanga , kufuatia mauaji ya wanafunzi 32 katika chuo hicho hapo jana.

Baadhi ya ndugu waliopoteza jamaa zao katika mauaji hayo
Baadhi ya ndugu waliopoteza jamaa zao katika mauaji hayoPicha: AP

Bado kuna utata mkubwa juu dhamira ya mtu aliyefanya unyama huo ambao haujawahi kutokea nchini Marekani toka yalipofanyika mauaji ya kinyama kama hayo katika chuo kikuu cha Texas mnamo mwaka 1966 ambapo wanafunzi 14 waliuawa.

Taarifa kutoka Polisi hazijaweka bayana endapo mtu aliyefanya unyama huo alikuwa ni mwanafunzi wa chuo hicho ingawa kwa namna alivyotekeleza mauaji hayo ni mtu anayeonekana kuyajua vyema mazingira ya chuo hicho.

Lakini Zoma Ketos mwanafunzi kutoka nchini Ethiopia anayesoma katika chuo hicho , anasema mtu aliyefanya mauaji hayo inasemekana ni mwanafunzi ingawa alikuwa hafahamiki sana chuoni hapo .

Baadhi ya wanafunzi wengi katika chuo hicho wametoa lawama zao kwa uongozi wa chuo hicho kwa kusema kuwa hawakupewa tahadhari yoyote baada ya kupata habari kwa njia ya barua pepe wakati tukio la kwanza la mauaji likiwa limefanyika.

Katika tukio hilo la kwanza muuaji aliwaua wanafunzi wawili waliokuwa bwenini kabla ya kuingia darasani ambako aliwaua wanafunzi wengine 29 akiwemo muhadhiri kutoka India.

Mwanafunzi mmoja Erin Mabry amesema ulipita muda wa masaa mawili kati ya tukio la kwanza na lile la pili wao bila ya kuwa na habari ya kile kinachoendelea chuoni hapo.

Lakini madai hayo ya wanafunzi yanapingwa na Rais wa chuo hicho Charles Steja ambaye amesema hawakua wakifahamu hatari iliyokuwapo katika chuo hicho.

"Tunaweza kufanya maamuzi kutokana na taarifa tulizokuwa nazo kwa wakati huo. Huna masaa ya kufikiria kwa muda huo" aliongeza bwana Steja.

Wakati huo huo Rais George Bush wa Marekani amesema amesikitishwa na kitendo cha mauaji ya wanafunzi hao na kusema serikali yake itafanya kila iwezalo kupata kiini cha kitendo hicho.

Amesikitishwa vitendo hivyo kutokea katika taasisi za elimu na kusema

Wakati Majina ya wanafunzi waliopoteza maisha yakiwa hayajatolewa polisi imesema mtu anayeshukiwa kufanya mauaji hayo alijiua baada ya matukio hayo.

Kufuatia mauaji hayo wanafunzi wengine 15 wamejeruhiwa vibaya walipokuwa wakijaribu kumzuia mtu huyo kuingia katika vyumba vya madarasa yao.