1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala bora Afrika unaimarika polepole

29 Septemba 2014

Utawala bora katika nchi za bara la Afrika unaimarika kwa kasi ndogo ambapo Somalia imeorodheshwa kama nchi ya chini kabisa katika faharasi ya utawala bora ya kila mwaka iliyotolewa leo.

Pressekonferenz der Mo Ibrahim Stiftung am 14. Oktober 2013
Picha: Mo Ibrahim Foundation

Lakini pia cha kushangaza ni kuwa faharasi hiyo ya mwaka wa 2014 ya Wakfu wa Mo Ibrahim inaonyesha kuwa nchi zilizofanya vyema hapo awali, zimeshuka angalau katika kipengele kimoja katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kwa mujibu wa vipengele vyote vinne vya faharasi au kielelezo cha utawala bora ya Mo Ibrahim ya mwaka huu, yaani usalama na utawala wa kisheria, ushiriki na haki za binaadamu, nafasi endelevu za kiuchumi na maendeleo ya watu, Somalia imerodheshwa ya mwisho kabisa.

Nembo ya Wakfu wa Mo Ibrahim

Mauritius imechukua nafasi ya kwanza, ikifuatwa na visiwa vya Cape Verde, Botswana, Afrika Kusini na Ushelisheli, nchi ambazo zote zilikuwa katika kundi la tano bora mwaka jana.

Orodha hiyo ya viwango inatokana na zaidi ya vigezo 100 kutoka vyanzo huru 30 vya barani Afrika na kimataifa. Mo Ibrahim, tajiri mkubwa wa kampuni ya mawasiliano nchini Sudan, ambaye ni muasisi wa wakfu huo, amepongeza ukweli kwamba 13 kati ya nchi 52 zimeimarika katika uongozi jumla pamoja na uongozi wa kisiasa, kijamii na kiuchumi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. "Kinachofurahisha kuhusu kuimarika huku ni kuwa kumekuja baada ya kipindi cha matukio mabaya. Nchi hizi zilikuwa zinashuka, lakini zikaanza tena kupanda, pengine baada ya kumalizika migogoro, au kuitatua migogoro, lakini inatia moyo kuubadilisha mkondo huo".

Rais wa Zamani wa Botswana Festus Mogae alishinda Tuzo ya Mo Ibrahim mwaka wa 2008Picha: picture-alliance/ dpa

Lakini amezionya nchi zilizofanya vyema kuendelea kulinda mafanikio yao ya uongozi bora. "Nchi hizo tano kila mwaka zimekuwa juu ya orodha yetu tangu tulipoanza miaka 13 iliyopita, na kila mara zinaimarika kwa jumla. Lakini tukiangalia kwa undani zaidi, nchi hizo tano bora zimeanza kuonyesha mapungufu kiasi katika baadhi ya vitengo".

Mauritius, Afrika Kusini na Ushelisheli zilianguka katika kipengele cha usalama na utawala wa kisheria, Cape Verde ikazembea katika kipengele cha maendeleo ya watu nayo Botswana ikashindwa kufanya vyema katika suala la maendeleo endelevu ya kiuchumi.

Afrika Kusini pia imerudi nyuma hatua kadhaa kuhusiana na suala la haki za binaadamu. Nchi zilizoimarika katika suala jumla la uongozi ni Cote d'Ivoire, Guinea, Niger, Zimbabwe na Senegal, wakati hali ikiwa mbaya zaidi katika mataifa ya Misri, Libya, Guinea-Bissau, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mali.

Kanda ya Kusini mwa Afrika ilipata alama nyingi zaidi katika kiwango cha kikanda, huku Namibia na Lesotho zikijiunga na Mauritius, Botswana na Afrika Kusini katika kundi la nchi kumi bora. Nalo eneo la Afrika ya Kati limekuwa la chini kabisa, ambapo Jamhuri ya Afrika ya Kati ilikuwa mbele ya Somalia katika orodha ya jumla ya viwango, na Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea ya Ikweta na Kongo – Brazaville pia zikiwa miongoni mwa nchi kumi zilizoshika mkia katiak ripoti hiyo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW