Utawala Mali wasitisha shughuli za vyama vya siasa
11 Aprili 2024Akisoma taarifa iliyotolewa na kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita, msemaji wa serikali Kanali Abdoulaye Maiga amesema shughuli za vyama vya siasa na shughuli za kisiasa zimesitishwa kote nchini Mali, hadi pale itakapoamuriwa tena na kusisitiza kuwa hatua hiyo inahitajika ili kudumisha utulivu wa umma.
Kanali Maiga alitangaza mbele ya waandishi wa habari, amri hiyo iliyoamulia na Baraza la Mawaziri na kusema vitendo vya uasi vinavyoendeshwa na vyama vya siasa na washirika wake vinaongezeka na kwamba hawawezi kufanya mazungumzo muhimu ya kitaifa yaliyoanzishwa Desemba 31 na Kanali Goïta, huku kukiwa na hali ya mkanganyiko na machafuko.
Soma pia:Mzozo wa Sahel waendelea kufukuta
Amri hiyo inatolewa baada ya zaidi ya vyama 80 vya kisiasa na mashirika ya kiraia mnamo Aprili mosi, kutoa taarifa ya pamoja ya kutaka kufanyike uchaguzi wa rais haraka iwezekanavyo ili kukomesha utawala wa kijeshi.
Taarifa hiyo ya pamoja ya vyama vya upinzani ambayo ilitiwa saini na watu zaidi ya 20, ukiwemo muungano mkubwa wa upinzani na chama cha rais wa zamani aliyepinduliwa Ibrahim Boubacar Keïta, ilisisitiza kuwa watatumia njia zote za kisheria na halali kurejesha utaratibu wa kawaida wa kikatiba katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Hali ya kisiasa na kiusalama katika eneo la Sahel
Mali imetawaliwa na wanajeshi tangu mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021, huku hali mbaya ya usalama ikichangiwa na mzozo wa kibinadamu na kisiasa. Pia, sauti za upinzani zimekandamizwa kwa kiasi kikubwa chini ya utawala huo wa kijeshi ambao mwezi Machi ulipiga marufuku shughuli za muungano mpya wa upinzani kwa madai kuwa ulikuwa ukitishia kuvuruga utulivu wa umma.
Soma: Utawala wa kijeshi Mali wazuia shughuli zote za vyama vya siasa
Mwezi Juni mwaka 2022, serikali hiyo ya kijeshi iliahidi kuwa uchaguzi wa rais utafanyika Februari mwaka huu na mamlaka kurejeshwa kwa watawala wa kiraia mnamo Machi 26, lakini uchaguzi huo uliahirishwa na hadi sasa utawala wa kijeshi haujaweka wazi nia na mipango yake.
Tangu mwaka 2012, Mali imekuwa ikikabiliana na uasi wa makundi ya kigaidi yenye mafungamano na Al-Qaeda na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Katika taarifa hiyo, Kanali Maïga alieleza pia kuwa wanaendelea na mapambano dhidi ya makundi ya wanajihadi wenye silaha pamoja na vikundi vya jamii ya Tuareg wanaodai uhuru wao.
Soma pia: Viongozi wa ECOWAS wakutana kujadili muelekeo wa mataifa yaliyo chini ya utawala wa kijeshi
Tangu kunyakua mamlaka mnamo mwaka 2020, serikali ya kijeshi imesitisha mahusiano na washirika wake wa Ulaya ikiwemo mkoloni wake wa zamani Ufaransa, na badala yake kuimarisha uhusiano wa karibu na Urusi. Pia, utawala huo ulilazimisha ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Maitaifa nchini humo MINUSMA kuondoka.
Kitendo cha wanajeshi kuchukua madaraka nchini Mali, kilichochea pia mapinduzi katika mataifa jirani ya Burkina Faso mwaka 2022 na Niger mwaka 2023. Nchi hizo tatu za Sahel zinazoongozwa na jeshi zimeunda muungano na kuamua kujiondoa kwenye Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.
(Vyanzo:AP,AFP)