1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa Biden waiwekea Korea Kaskazini vikwazo

13 Januari 2022

Utawala wa rais wa Marekani Joe Biden umeiwekea Korea Kaskazini vikwazo vya kwanza kufuatia mipango yake ya silaha.

Nordkorea | Raketentests
Picha: YONHAPNEWS AGENCY/picture alliance

Hatua hiyo imejiri baada ya Korea Kaskazini kufanya majaribio mawili ya makombora tangu wiki iliyopita.

Vikwazo hivyo vya Marekani vinawalenga raia sita wa Korea, mmoja wa Urusi na pia kampuni moja ya Urusi.

Marekani imesema walengwa walihusika katika kununua vifaa kutoka Urusi na China ambavyo Korea Kaskazini inatumia katengeneza silaha.

Soma pia:

Korea Kaskazini yafyatua kombora kuelekea Mashariki

Mataifa makubwa kinyuklia yaahidi kupunguza silaha za nyuklia

Korea Kaskazini yafanya jaribio la kombora kwa kutumia nyambizi

Wizara ya fedha ya Marekani imesema lengo la vikwazo hivyo ni kuizuia Korea Kaskazini kuendelea na mipango hiyo yake na kuzuia jaribio lolote la kujiongezea teknolojia za silaha.

Marekani pia imependekeza kwamba watu watano miongoni mwa waliowekewa vikwazo wajumuishwe kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo vya kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Pendekezo hilo litahitaji kuridhiwa na nchi 15 wanachama wa kamati ya vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.

Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje nchini Marekani Ned Price amesema Marekani ingali imejitolea kutafuta diplomasia na Korea Kaskazini.Picha: Olivier Douliery/AP Photo/picture alliance

Tangu Biden alipochukua mamlaka kuiongoza Marekani Januari mwaka uliopita, utawala wake umekuwa ukijaribu bila mafanikio, kuishawishi Korea Kaskazini kwa njia ya mazungumzo kuachana na mipango yake ya makombora na mabomu ya nyuklia.

Marekani yaishutumu Korea Kaskazini kutotii maafikiano ya UN

"Hii ni mikakati muhimu ya kubana mipango ya Korea Kaskazini ya makombora na nyuklia. Na ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kutuma ujumbe mkali wa pamoja kwamba Korea Kaskazini sharti ikomeshe uchokozi. Ni lazima itemize ahadi zake kulingana na maafikiano ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ishiriki kikamilifu katika mazungumzo. Hadi sasa hatujaona hayo yote yakitekelezwa,” amesema Price.

Wizara ya Fedha ya Marekani imesema vikwazo hivyo vimetolewa kufuatia majaribio sita ya kufyatua makombora ambayo yamefanywa na Korea Kaskazini tangu mwezi Septemba mwaka uliopita, hatua zilizokiuka maafikiano ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kutokana na jaribio hilo, Kim alidai ni juhudi za kuongeza uwezo wa nchi yake kinyuklia na ulinzi kivita.Picha: KCNA/KNS/AFP

Korea Kusini ambayo imekuwa ikiishinikiza Marekani kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini, imesema haiamini kwamba hatua iliyochukuliwa na Marekani inamaanisha utawala wa Biden umekaza msimamo wake, bali unaakisi msimamo uliopo kwa sasa wa Marekani kwamba vikwazo pia ni muhimu, pamoja na mazungumzo. Hayo ni kulingana na msemaji wa msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini.

Ujumbe wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa, Urusi na China hazikutoa kauli kuhusu hatua ya Marekani licha ya maswali kutoka kwa wanahabari.

Shirika la habari la Korea Kaskazini lilisema kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un alishuhudia ufyatuliaji kombora la kasi kubwa siku ya Jumanne. Huo ukiwa urushaji kombora wa pili katika kipindi cha wiki moja.

Kutokana na jaribio hilo, Kim alidai ni juhudi za kuongeza uwezo wa nchi yake kinyuklia na ulinzi kivita.

(RTRE, APE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW