1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa kijeshi Burkina Faso kuhudumu miaka 3

Hawa Bihoga
1 Machi 2022

Kiongozi wa utawala huo ambae aliongoza mapinduzi ya kumuondoa Rais Marc Kabore mwezi Januari Luteni Kanal Herri Paul Damiba ametia saini mkataba huo kwenye mkutano wa kitaifa uliofanyika katika mji mkuu Ouagadougou.

Burkina Faso | Demonstration zur Unterstützung der Militärjunta
Picha: Olympia de Maismont/AFP/Getty Images

Mkutano huo wa kitaifa ulihusisha wanasiasa, vyama vya siasa, vyama vya wafanyakazi, vijana na wanawake, pamoja na watu waliokimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi ambayo yameikumba Burkina Faso tangu 2015.

Mkataba huo pia unaeleza kuwa rais wa kipindi cha mpito hastahiki kushiriki uchaguzi wa rais, wabunge na manispaa ambao utaandaliwa ili kutamatisha  utawala huo wa mpito.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa waeleza wasiwasi juu ya Burkina Faso

Mbali na mambo mengine mkataba huo unaainisha pia serikali hiyo ya mpito itakuwa na jukumu la kukomesha masuala ya ugaidi, kurejesha uadilifu kadhalika kutoa majibu madhubuti na ya haraka kutokana na mzozo wa kiuchumi na kibinadamu unaosababishwa na ukosefu wa usalama.

Utawala wa mpito unahitaji muda kuleta utulivu

Tume iliyoandaa mkataba huo ambao umeruhusu serikali hiyo ya kijeshi kusalia mamlakani kwa kipindi cha miezi 36, ilipendekeza kipindi cha mpito cha miaka miwili na nusu, kwa hoja kuwa utawala huo ulihitaji takriban miaka miwili ili kuleta utulivu katika taifa hilo la Afrika Magharibi na kuandaa mchakato wa uchaguzi.

Kiongozi wa mapinduzi Burkina Faso Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo DamibaPicha: Radiodiffusion TÈlÈvision du Burkina/AFP

Burkina Faso pamoja na majirani zake Mali na Niger wanaelekeza jitihada katika kuzuia mashambulizi ya wanamgambo wenye kumiliki silaha  wanaofungamana na kundi la Al-Qaeda na lile la dola la kiislamu ambao wamefanya mauaji ya watu huku mamia kwa maelfu wameyakimbia makazi yao katika eneo hilo la Sahel.

Soma zaidi:Jeshi laahidi kurejesha usalama Burkina Faso

Kiongozi wa chama kukuu cha upinzani ambaye alishika nafasi ya pili katika kinyang'anyiro cha urais mwaka 2020 Eddie Komboigo, ameridhia mkataba huo. Amesema si kila mmoja ataridhishwa na mkataba huo wa mpito lakini ilikuwa ni makubaliano.

Aidha kiongozi huyo kutoka chama cha upinzani ameutaka utawala huo wa kijeshi kufanya mazungumzo na viongozi wa kikanda na washirika wa kimataifa wote waweze kukubaliana juu ya kurefushwa kwa uongozi huo wa mpito.

Raia katika maandamano ya kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi Burkina FasoPicha: Sophie Garcia/AP/picture alliance

Burkina Faso, ilisimamishwa kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, na Umoja wa Afrika, jumuia zote zikitoa wito wa kurejea haraka kwa utaratibu wa kikatiba, huku Marekani ikisitisha msaada wa takriban dola milioni 160 kutokana na mapinduzi hayo.

Chanzo:Reuters, AFP