Utawala wa kijeshi Mali waomba msaada
31 Machi 2012Jeshi la Mali lilisema kuwa limewaondoa wanajeshi wake katika miji miwili ya Kaskazini mwa nchi hiyo, saa chache baada ya waasi wa Kituareg kuwatimua kutoka mji muhimu wa Kidal. Kwa mujibu wa taartifa iliyotolewa na jeshi, vikosi viliondoka katika miji ya Ansogo na Bourem ili kuimarisha nafasi zao katika mji wa Gao. Gao ni mji mkubwa Kaskazini mwa Mali ambao ungali mikononi mwa jeshi la Mali linaloongoza nchi kwa sasa.
Hali sasa ni mbaya
Ombi la Sanogo lilitolewa jana wakati ambapo uongozi wa jeshi hilo uliodumu wiki moja, na ambao tayari umetengwa na washirika wake wa nje unakabiliwa na uwezekano wa kuwekewa vikwazo vya kiuchumi kutoka kwa nchi jirani vinavyoweza kuikwamisha nchi hiyo. Nchi hizo zinataka kurejeshwa kwa utawala wa kikatiba nchini humo.
Kiongozi wa mapinduzi Kapteni Sanogo aliwaambia waandishi habari katika ikulu ya rais ambayo sasa ndiyo makao makuu ya kijeshi kuwa waasi wanaendelea kuishambulia nchi yao na kuwasumbua raia. Aliongeza hali sasa ni mbaya, jeshi linahitaji msaada kutoka kwa marafiki wa Mali ili kuwaokoa wananchi na kuilinda himaya ya nchi hiyo. Baada ya mapigano makali, waasi wa Kituareg pamoja na kundi moja la Kiislamu lililojihami ambalo linawaunga mkono waasi hao, waliingia mji wa Kidal, ambao ni kilomita 1,000 kutoka mji mkuu Bamako.
Mapigano kuendelea
Katika tuvuti yake, kundi la Azawad National Liberation Movement MNLA lilisema litaendelea na mashambulizi dhidi ya miji mingine miwili mikuu katika eneo hilo ili kuwaondoa wanajeshi wa Mali. Wapiganaji wa kundi la MNLA wanashirikiana na wanamgambo wa Kiislamu wa Ansar Dine yaani “Walinzi wa Imani” katika lugha ya Kiarabu.
Mashambulizi ya Tuareg yamesababisha takribani watu 200,000 kukimbia makwao katika eneo la kaskazini mashariki mwa Mali ambalo pia ni maarufu kwa ulanguzi wa silaha na dawa za kulevya. Kutwaliwa kwa mji wa Kidal, ambao ndio mji mkuu wa jimbo la Kaskazini Mashariki unaopakana na Niger na Algeria ni mafanikio makubwa kwa waasi hao ambao tayari wametwaa udhibiti wa miji mingine mikuu ya Tessalit na Aguelhok katika mkoa huo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mtullya Abdu