Utawala wa kijeshi wa Niger wawakamata maafisa wa serikali
31 Julai 2023Taarifa iliyotolewa na chama cha Bazoum cha PNDS imesema mawaziri wanne ambao ni wa mafuta, madini, uchukuzi na wa mambo ya ndani, wametiwa nguvuni na mamlaka za kijeshi.
Chama hicho pia kimesema kiongozi wake wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Fourmakoye Gado, na waziri mmoja wa zamani nao amekamatwa.
Chama cha PNDS kimetaka kuachiwa huru kwa maafisa hao mara moja kikisema taifa hilo limo kwenye hatari ya kutumbukia kwenye utawala kidikteta.
Soma zaidi: Vikwazo vya kiuchumi vya ECOWAS kuwaathiri raia wa Niger
Kukamatwa kwao kumetokea baada ya tangazo lililotolewa na utawala wa kijeshi la kuamuru mawaziri wote na wakuu wa taasisi za serikali kukabidhi magari yote ya umma ifikapo leo mchana.
Utawala wa Bazoum ulipinduliwa Jumatano iliyopita na maafisa wake wa kikosi cha ulinzi, na tangu wakati huo kiongozi wa kundi hilo la wanajeshi waasi, Abdourahamane Tiani, amejitangaza kuwa kiongozi mpya wa Niger.