Utekaji nyara wamalizika Algeria
22 Januari 2013Mateka 21 wameuwawa wakati eneo hilo lilipokuwa limezingirwa , hali iliyotokana na watu wenye silaha wenye mafungamano na kundi la al-Qaeda waliposhambulia kituo cha kukusanyia gesi asilia cha In Amenas ndani ya eneo la jangwa la sahara mapema alfajiri siku ya Jumatano, imesema wizara ya mambo ya ndani.
Wateka nyara 32 pia wameuwawa, na kikosi maalum cha jeshi la Algeria kilifanikiwa kuwaacha huru wafanyakazi 685 raia wa Algeria pamoja na wafanyakazi kutoka nchi za nje wapatao 107, taarifa hiyo imesema.
Raia wa kigeni wauwawa
Miongoni mwa wale waliouwawa kuna idadi ambayo haijulikani ya raia wa kigeni , ikiwa ni pamoja na wanaotoka Uingereza, Ufaransa, Romania na Marekani, na wengi bado hawajulikani waliko.
Kampuni ya uhasindisi kutoka Japan ya JGC Corp. imesema leo kuwa Wajapani 10 na wafanyakazi wengine saba wa kigeni bado hawajulikani waliko, lakini imethibitisha kuwa wafanyakazi 61 miongoni mwa 78 wako salama.
Wateka nyara wakiongozwa na Mokhtar Belmokhtar raia wa Algeria , ambaye ni kamanda wa zamani wa kundi la al-Qaeda katika eneo la Afrika ya kaskazini , wamewauwa watu wawili katika basi, Muingereza na raia wa Algeria , kabla ya kuwakamata mamia ya wafanyakazi mateka wakati walipokishambulia kituo hicho cha gesi asilia.
Kundi la Belmokhtar la "Signatories in Blood", waliotia saini kwa damu limekuwa likidai kumalizwa kwa uingiliaji kati kijeshi wa Ufaransa dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu katika nchi jirani ya Mali.
Kiongozi huyo wa kundi hilo la wapiganaji ameonya katika matamshi aliyotoa na kutangazwa jana jumamosi kuwa ataripua kituo hicho cha kusafisha gesi iwapo jeshi litafika karibu na kituo hicho.
Katika matamshi yake yaliyotangazwa na shirika la habari la Mauritania,kamanda wa kikosi cha Al-Mulathameen , Abdul Rahman al-Nigeri kutoka Niger amesema siku ya Alhamis wakati jeshi la Algeria lilipozingira maeneo ya wapiganaji wake.
Nigeri anasemekana kuwa kiongozi wa ngazi ya juu kwa kiongozi mkuu wa wateka nyara Belmokhtar. Katika shambulio la Jumamosi , jeshi la Algeria liliwakamata magaidi 11, na kundi hilo la kigaidi liliuwa mateka wao saba raia wa kigeni.
Mauzo ya nje hayakuathirika
Wakati huo huo Algeria haijapunguza mauzo yake ya nje ya gesi baada ya kuanza kwa mzozo huo wa utekaji nyara, wizara ya nishati ya nchi hiyo imesema.
"Washirika wetu hawajaathirika kutokana na hali hiyo. Hatukupunguza mauzo yetu ya nje ya gesi, tumeweza tu kujaliza upungufu huo kwa uzalishaji kutoka katika maeneo mengine ya nchi, " shirika la habari la APS limemnukuu Youcef Yousfi.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Stumai George