1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utekelezwaji wa mkataba wa nyuklia Iran wazua lawama

John Juma15 Juni 2016

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah ailaumu Marekani kujikokota katika kuondoa vikwazo kinyume na mkataba ulivyo.Waziri wa masuala ya kigeni wa Marekani John Kerry asema vikwazo vimelegezwa.

Mazungumzo kuhusu nyuklia.
Mazungumzo kuhusu nyuklia.Picha: Reuters/K. Lamarque

Waziri wa masuala ya kigeni wa Marekani John Kerry kwa mara nyingine amekutana na mwenzake wa Iran kujadili malalamiko ya Iran kuwa haipati nafuu inayostahili kuhusu vikwazo ilivyowekewa licha ya nchi hiyo kufikia makubaliano na madola makubwa kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Mkutano wa Kerry na Mwenzake Mohammed Javad Zarif mjini Oslo, umejiri siku moja tu baada ya kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, kuilaumu Marekani kuwa haitimizi makubaliano ya kulegeza vikwazo vya awali ilivyowekewa Iran kuhusu mipango yake ya nyuklia, tofauti na mkataba unavyohitaji.

Wawili hao wamejadili utekelezwaji wa mkataba huo wa nyuklia, yakiwemo masuala yanayogusia sekta ya benki na kuondolewa kwa vikwazo vya kinyuklia. Kerry amezungumzia umuhimu wa Iran kutumia ushawishi wake dhidi ya Syria kuhakikisha misaada inafikishwa kwa wanaoathirika na pia kusitishwa kwa uhasama, huku akiongeza kuwa uvumilivu wa Marekani dhidi ya Syria, Urusi na washirika wake unayoyoma.

Uvumilivu wa Marekani unayoyoma

Kerry Amesema "Ni bayana kuwa usitishwaji wa uhasama nchini Syria unafifia na katika hatari. Ni muhimu kwa usitishwaji kamili wa mapigano kuafikiwa. Tunajua hilo, hatuna maruweruwe. Urusi inapaswa kuelewa kuwa uvumilivu wetu si wa milele, kwa sasa umeyoyoma kuhusu ikiwa Assad atawajibishwa. Tumejiandaa kuwajibisha wapinzani ambao pia wanachezeana shere kuendeleza ghasia na kuvunja mkataba wa usitishwaji mapigano."

John Kerry na Javad Zarif .Picha: Getty Images/AFP/D. Reuter

Marekani inasema vikwazo dhidi ya Iran vimelegezwa na kuwa lalama za Iran zinatokana na hofu za jamii za kimataifa kufanya biashara na nchi hiyo kwa sababu tofauti, ikiwemo majaribio ya makombora, ushirikiano wake na Syria, kupinga baadhi ya makundi ya Israel na kanuni mbaya katika idara yake ya benki.

Mnamo Jumanne, kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema, Iran imetimiza matakwa ya mkataba, lakini Marekani inajikokota kuondoa vikwazo dhidi ya sekta za benki na bima na kuachilia mali za Iran. Aidha, Ayatollah ameelezea upinzani wake dhidi ya kuijongelea zaidi Marekani na mataifa ya magharibi akisema yamesalia kuwa wakali dhidi ya Iran. Ameongeza kuwa endapo rais mpya wa Marekani atafutilia mbali mktaba huo wa nyuklia, Iran itaiwashia moto.

Wakati uo huo Zarif amesema dhana zilizosalia kuhusu vikwazo vilivyokuwepo zinazuia benki za Ulaya na Asia kufanya biashara halali na Iran.

Mwandishi: John Juma/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga