1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utendaji wa Magufuli wazua mjadala mzito Tanzania

16 Aprili 2021

Nchini Tanzania kuna mgawiko kufuatia kujitokeza kwa kambi mbili kinzani, zinazojipambanua hadharani kutetea utawala wa aliyekuwa rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli dhidi ya wale wanaoukosoa utawala wake.

Tansania Präsident John Magufuli verstorben
Picha: AFP

Hali hiyo inashuhudiwa zaidi bungeni ambako chama tawala CCM kinalitawala bunge hilo lakini michango ya wabunge wake inatofautina kwa kiwango kikubwa na wakati mwingine wakitupiana vijembe vya waziwazi.

Ingawa baadhi ya wakosoaji wa utawala wa Hayati Magufuli wakati mwingine hutoa michango yao katika hali ya mafumbo, lakini kuna idadi kadhaa ya wabunge kauli zao ni zile za moja kwa moja zinabainisha namna wasivyoridhishwa na utendaji wa kiongozi huyo aliyekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano na miezi mitano hivi.

soma zaidi: Maoni: Magufuli, rais aliyependwa kama alivyochukiwa

Baadhi ya wabunge katika bunge la TanzaniaPicha: DW/S. Khamis

Kwa mfano, mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba alionekana kuwa mwangalifu zaidi wakati akijadili jambo hilo la magawanyiko na mwishowe hakuonyesha msimamo wake wa moja kwa moja kama yuko upande wanaotetea utawala wa Magufuli au wale wanaotoa dukuduku lao la ukosoaji.

"Kazi aliyotufanyia rais magufuli naweza kuichukulia kama vile ametushonea nguo, nzuri kabisa ya kupendeza, akijitokeza mtu akasema katika hii nguo kifungo kimelegea hebu tukiweke vizuri isionekane huyu mtu ni msaliti," alisema Januari Makamba

Baadhi ya wabunge wasema hawatokubali Magufuli asemwe vibaya

Baadhi ya wabunge wamejipambanua wazi wazi kwa kauli zao wakisema kamwe hatakuwa tayari kuona jina la Hayari Rais Magufuli likisemw avibaya na wao waendelee kukaa kimya. Wabunge kama kina Livingstone Lusinde ni sehemu ya kundi hilo la wabunge.

"Leo asemwe vibaya si tupo, leo Magufuli asemwe vibaya hata arubaini haijaisha spika hili jambo halikubaliki, hawa watu washike adabu na adabu ziwashike hatutaki warudie tena mambo ya kipuzi kama haya," alisema Livingstone Lusinde

soma zaidi: Hayati Magufuli aagwa kwa majonzi makubwa Mwanza

Kujitokeza kwa hali hiyo hasa ndani ya chama hicho tawala CCM, kunazua maswali mengi namna utawala wa Magufuli ulivyowagusa wanasiasa hao na wananchi kwa ujumla.

Wataalamu wasema kiongozi kusema ni jambo la kawaida

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakiijadili hali hiyo kwa mitazamo tofauti ingawa wengi wao wanaona kwamba hali hiyo inatoa picha halisi kuhusu utawala huo uliopita namna ulivyoendesha mambo yake.

Aliyekuwa rais wa Tanzania Hayati John MagufuliPicha: Daniel Hayduk/AFP

Gwandumi Mwakatobe ni mchambuzi na mtu anayefuatilia kwa karibu hali ya siasa nchini Tanzania na eneo la Afrika Mashariki, yeye anasema kiongozi sio mkamilifu kusemwa ni jambo la kawaida.

"Pamoja na kuwepo uhuru wa kutoa maoni ambayo mtu anayo mtu yeyote ambae anashika madaraka, sirahisi akaweza kuwa mkamilifu, hawezi kuwa ni malaika lazima atakuwa na dosari zake ndio ubinaadamu huo uliopo, kitu pekee tunachoweza kufanya ni kusahihisha mifumo ambao tunaona haikuwa sahihi katika utawala uliopita," alisema bwana Mwakatobe.

Wakati wote wa utawala Hayati Rais Magufuli, vyama vya upinzani ndivyo vilivyokuwa daima vikilalamika zaidi juu ya kile ilichokuwa ikisema kubinywa kwa uhuru wa maoni na shughuli za siasa.

Mwandishi: George Njogopa DW Dar es Salaam

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW