1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uteuzi wa waziri mkuu mpya Madagascar wazua mjadala

Hilda Hasinjo, Sylvanus Karemera21 Oktoba 2025

Siku moja baada ya kiongozi wa kijeshi nchini Madagascar Kanali Michael Randrianirina kumteua waziri mkuu mpya Herintsalama Rajaonarivelo vijana wa nchi hiyo wametangaza tena nia ya kumpinga waziri mkuu mpya mteule.

Kanali Michael Randrianirina akipongezwa na majaji wa mahakama ya katiba baada ya kuapishwa kuwa rais
Kanali Michael Randrianirina aliapishwa kuwa rais wa MadagascarPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Hisia zilikuwa kali katika mji mkuu wa Madagascar, Antananarivo mara baada ya uteuzi wa Waziri Mkuu mpya na mfanyabiashara maarufu Herintsalama Rajaonarivelo. Ingawa yeye ni sura mpya na kiungo katika siasa za Madagascar, hisitoria yake ya kisiasa mbele ya vijana wanaotaka mageuzi na vyama vya wafanyakazi vinavyotaka mapinduzi kwa pamoja vinaleta wasiwasi.

Mara tu jina la Waziri Mkuu huyo lilipotangazwa na Katibu Mkuu wa Ikulu ya Madagascar, picha na taarifa kuhusu yeye zilienea kwa haraka mitandaoni. Katika baadhi ya picha anaonekana akiwa pamoja na wanasiasa wa utawala uliopita huku akimpongeza rais wa zamani Andry Rajoelina.

Picha hizo pia zinamuonyesha katika picha akiwa na tabasamu huku akiwa pamoja na mfanyabiashara maarufu nchini humo Mamy Ravatomanga. Hili limezidisha hali ya wasiwasi miongoni mwa vijana ambao wanasema kiongozi huyu wa kijeshi anaonekana kupuuza majina yao mawili waliyokuwa wameyapendekeza tokea mwanzo. Kiongozi wa vuguvugu hilo la vijana Randrianaivo Aimé Nicolas amesema: ''Tuna mashaka na wasiwasi kuhusu chaguo hili, hata hivyo bado tunaamini katika mazungumzo na mwisho kuchukua maamuzi ya pamoja. Kwa hiyo tutafanya kikao chetu cha pamoja hii leo Jumanne kutathmini hali hii kisha baadaye tutachukua uamuzi wa pamoja na tutatoa tangazo baada ya mkutano huu.''

Maandamano ya vijana wa Gen Z nchini Madagascar yalisababisha mapinduzi ya kijeshi Picha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Kwa upande mwingine vyama vya wafanyakazi ambavyo daima huwa katika hali ya malalamiko navyo vinaona ni kama juhudi zinazochukuliwa na utawala mpya ni kama nusu ya kile walichokitarajia. Hata hivyo, waziri mkuu mpya aliwahi kushika nyadhifa muhimu kama vile kuwa mkuu wa chama cha waajiri cha wenye viwanda vidogo vidogo kwa muda wa miaka 10 na baadaye akashikilia nafasi za juu katika Shirika la Bima za Umma nchini Madagascar.

Kwa upande mwingine uzoefu huu wa waziri mkuu mpya ndiyo umemfanya Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyabishara nchini humo Barson Rakotomanga, kutangaza kwamba ana matumaini kuwa sasa mabadiliko yanakwenda kutokea nchini Madagascar.

''Sisi, waandamanaji, hasa vyama vya wafanyakazi vilivyoongoza harakati ambazo zilisababisha Waziri Mkuu mpya kuteuliwa katika nafasi hii, tunatarajia mageuzi makubwa ya mfumo wa ajira. Kwa hiyo pia tunatarajia kutoa ushirikiano wa karibu, hasa kuhusu huduma za kijamii, afya na malipo ya pensheni.''

Kulingana na waziri mkuu mteule shughuli za kuunda serikali mpya zinaanza leo Jumanne. Na tayari Rais wa mpito Kanali Michaël Randrianirina, ameahidi kuwa na serikali yenye uwazi ambayo itawapa sauti ya kutosha vijana wa Madagascar.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW