1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utulivu warejea kwenye mpaka wa Poland na Belarus

17 Novemba 2021

Hali ya utulivu imerejea kwenye mpaka kati ya Poland na Belarus siku moja tangu vikosi vya usalama vya Poland vilipotumia maji ya kuwasha kuwakabili wahamiaji waliokwama upande wa Belarus.

Belarus Grenze zu Polen | Migranten | Zuspitzung der Lage
Picha: Leonid Shcheglov/BelTA/AP/picture alliance

Duru kutoka eneo la mpaka wa Kuznica-Bruzgi  zinasema utulivu umeshuhudiwa tangu Jumanne jioni baada kuzuka patashika kwenye eneo hilo ambako wahamiaji wamekusanyika upande wa Belarus wakijaribu kuingia kinyume cha sheria nchini Poland.

Idara ya polisi wa mpakani nchini Poland imeandika kupitia ukurasa wa Twitter kuwa wahamiaji wamerejea kwenye kambi iliyo karibu na mpaka huo baada ya vurumai ya jana mchana.

Wamesema kulikuwa na karibu wahamiaji 2,000 kwenye eneo hilo wakati makabiliano yalipotokea.

Ghasia kubwa ilizuka mapema Jumanne baada ya polisi ya Poland kuwarushia maji ya kuwasha wahamiaji waliokwama kwa wiki kadhaa kwenye mpaka huo wakilenga kuingia kwenye kanda ya Umoja wa Ulaya kupitia Poland.

Poland yatetea uamuzi wa kuwakabili wahamiaji 

Vurumai ilikuwa kubwa siku ya Jumanne Picha: Leonid Shcheglov/BELTA/AFP/Getty Images

Wizara ya Ulinzi ya Poland ilisema vikosi vyake vilichukua hatua hiyo kuwadhibiti watu waliokuwa wakirusha mawe na kuituhumu serikali ya Belarus kuwa iliwapatia baadhi ya wahamiaji mabomu ya kutoa machozi.

Mzozo kwenye eneo hilo uliokuwa ukifukuta tangu majira ya kiangazi umepamba moto mapema mwezi wakati maelfu ya wahamiaji, wengi kutoka mashariki ya kati wakiendelea kujikusanya kwenye maeneo tofauti ya mashariki ya Ulaya ili kutafuta hifadhi katika mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Umoja huo unailaumu serikali ya rais Alexander Lukashenko wa Belarus kwa kuwavutia na kuwasafirisha wakimbizi hao hadi kwenye mipaka na mataifa ya kanda hiyo.

Brussels inaamini Lukashenko anatumia mbinu hiyo kulipa kisasi vikwazo ilivyoweka dhidi ya Belarus kutokana madai ya udanganyifu kwenye uchaguzi wa mwaka uliopita.

Merkel akaliwa kooni kwa juhudi zake za kutafuta suluhu

Hali ya kiutu ni mbaya kwenye eneo la mpaka Picha: Oksana Manchuk/BelTA/dpa/picture alliance

Katika hatua nyingine mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Ulaya Dunja Mijatović hapo jana alifanya ziara kwenye kituo cha kuwasaidia wahamiaji kwenye mpaka kati ya Poland na Belarus.

Akiwa kwenye mji wa mpakani wa Michalowo alikoshuhudia hali ilivyo, Mijatovic amesema licha ya kuendelea kwa mzozo, Ulaya haipaswi kupuuza madhila wanayopitia wahamiaji ambao wengi hufika eneo hilo wakiwa na majereha mwilini na hakuna maeneo ya kutosha ya kuwapatia hifadhi.

Juhudi za kidiplomasia bado zinaendelea kutafuta majibu kuhusu mzozo huo. Rais Lukashenko wa Belarus jana alifanya mazungumzo na mshirika wake wa karibu rais Vlamidir Putin wa Urusi kujadili suala hilo la wahamiaji lakini hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu kile kilichoafikiwa.

Wakati hayo yakijiri ukosoaji unamwandama Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye siku ya Jumatatu alifanya mazungumzo na rais Lukanshenko kutafuta njia ya kutatua mzozo unaendelea.

Wanasiasa kadhaa nchini Ujerumani, wengine kutoka mataifa ya Umoja wa Ulaya pamoja na kiongozi wa upinzani wa Belarus wamemlaumu Merkel kwa kuzungumza na Lukashenko wakisema amekiuka msimamo wa Ulaya wa kutomtambua Lukashenko kama rais halali wa Belarus.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW