Uturuki: Duru ya pili ya uchaguzi na biashara na Afrika
24 Mei 2023Uturuki inatoa mchango mkubwa katika ushindani wa ushawishi kati ya madola yenye nguvu kiuchumi barani Afrika. Taifa hilo linajionyesha kama mshirika mbadala wa wakoloni wa zamani wa Ulaya - na limefanikiwa katika hili. Rais wa sasa Recep Tayyip Erdogan na uwekezaji wake wanakaribishwa kwa mikono miwili katika mataifa mengi ya Kiafrika.
Baada ya kukosa kwa asilimia ndogo ushindi wa moja kwa moja katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Mei 14, Rais Erdogan atakabiliana na mpinzani wake Kemal Kilicdaroglu katika duru ya pili Jumapili ijayo, kura ambayo inatazamiwa kufautiliwa kwa karibu na mataifa mengi ya Afrika.
Ongezeko kubwa la biashara
Mchambuzi kutoka shirika la ushauri la kimataifa la Development Reimagined, Ovigwe Eguegu, anasema ukubwa wa biashara kati ya Uturuki na Afrika unaongeza shauku barani humo juu ya mwelekeo wa kisiasa nchini Uturuki.
"Tumekuwa na enzi ya dhahabu tangu 2003 na ambayo inaendelea hadi hii leo. Kiwango cha biashara leo kinakaribia bilioni 45, kutoka bilioni 5.4 katika kipindi cha takriban miaka 20. Hilo ni ongezeko kubwa la biashara na bara hili," Eguegu aliiambia DW katika mahojiano.
Katika muktadha wa mtazamo jumla wa kiuchumi, biashara inachangia asilimia 9.3 ya mauzo ya nje ya Uturuki, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.4 katika muda wa miaka 20, hali inayoonyesha umuhimu wa uhusiano huu kwa pande zote mbili. Lakini Eguege anasema pia uhusiano huu ni mgumu kwa sababu unahusisha mataifa kadhaa.
Soma pia: Upinzani Uturuki wafungua kesi kupinga ushindi wa Erdogan
Kwa mfano, kulingana na Eguegu, kuna mauzo mengi ya samani kutoka Uturuki kwenda Nigeria kwa sababu bidhaa za watengenezaji samani wa Kituruki hazina ushindani barani Ulaya. Uturuki pia imekuwa mshirika wa kuvutia wa kibiashara katika kanda ya Kifaransa ya Afrika Magharibi, ambako mataifa yanapunguza uhusiano wao na mkoloni wa zamani wa Ufaransa.
Mkakati wa Uturuki kwa Afrika ni mpana
Mkakati wa Uturuki wa Afrika unazingatia maeneo mbalimbali, kuanzia hatua za ushawishi kama vile msaada kwa elimu na taasisi za kijamii na miradi ya vyombo vya habari hadi misaada ya kibinadamu, kwa mfano katika maeneo yenye njaa ya Somalia, na miradi ya miundombinu.
Makampuni ya ujenzi ya Uturuki yanafanya biashara nzuri barani Afrika kwa ujenzi wa barabara, madaraja, njia za reli, bandari, viwanja vya ndege na misikiti. Bara hilo pia linazidi kuwa muhimu kwa Uturuki kama msambazaji wa nishati na malighafi.
Mmoja wa washirika muhimu hapa ni Algeria, mojawapo ya wasambazaji muhimu wa malighafi wa Uturuki: Mnamo Novemba 2022, mipango ilitangazwa na nchi zote mbili kuanzisha kampuni ya pamoja ya uzalishaji wa mafuta na gesi.
Chini ya Erdogan, mkakati wa Uturuki kuelekea Afrika umechukua mwelekeo wa kijeshi wenye nguvu zaidi katika miaka ya hivi karibuni: Katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, Ankara sio tu inadumisha ujumbe muhimu wa kigeni, lakini pia kambi kubwa zaidi ya kijeshi nje ya nchi yake, Kambi ya Turksom ilyoko kwenye eneo lenye ukubwa wa kilomita nne.
Soma pia: Maoni: Erdogan adhihirisha utepetepe wa chunguzi wa maoni
Kulingana na wataalamu, Somalia ni mshirika muhimu zaidi wa Uturuki katika bara la Afrika, kutokana hasa na jiografia yake kwenye Pembe ya Afrika.
Idadi iliyoweka rekodi: Ziara za Erdogan barani Afrika
Kwa kipindi cha kiuchumi cha 2022/2023, Wizara ya Biashara ya Uturuki imeziainisha Misri, Ethiopia, Liberia, Nigeria na Afrika Kusini kama nchi walengwa, ambapo kwa mujibu wa Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TRT), uhusiano na nchi hizo unapaswa kukuzwa.
Hatimaye, Uturuki inalenga kubadilisha mahusiano yake ya kimataifa na kufungua masoko mapya, anasema Alex Vines, mkuu wa programu ya Afrika katika taasisi ya Chatham House ya mjini London. Na huo pia ni mojawapo ya vichocheo vikuu vya sera iliyozingatiwa katika muda wa miaka 20 iliyopita.
"Lakini ikiwa Erdogan atashinda katika duru ya pili na kuchafuliwa kwa muhula mwingine, tutaona mwendelezo wa sera ya Uturuki ya Afrika, sera ambayo imekuwa ikizingatiwa sana na kuimarishwa na Rais Erdogan," anasema Vines.
Hakuna kiongozi wa taifa aliyeizuru Afrika mara kwa mara kama Erdogan. Rais huyo ametemebelea mataifa 31 ya Afrika kuimarisha sera yake, na hii leo kuna mataifa 44 ya Afrika yalio na uwakilishi wa kidiplomasia mjini Ankara. Zaidi ya hayo, Uturuki ni miongoni mwa nchi zinazotoa misaada zaidi duniani.
Soma pia:Serikali ya Urusi yakanusha kujiingiza kwenye kampeini ya uchaguzi wa rais nchini Uturuki
Na ingawa iko chini ya shinikizo kubwa, ikiwa ni pamoja na baada ya tetemeko la ardhi katika nchi yake, kuna utamaduni wa ukarimu katika kukabiliana na migogoro ya kibinadamu na njaa katika Pembe ya Afrika, Vines anasema.
Uturuki: Mwamko wa kiuchumi
Katika muktadha wa uchaguzi, kampeni zimejikita zaidi kwenye masuala ya ndani, anasema Vines. Lakini ikiwa Erdogan ataibuka mshindi katika duru ya pili, tutaona mwendelezo wa sera ya Uturuki kwa Afrika, ambayo Rais Erdogan ameizngatia sana na kuiimarisha, kwa mujibu wa Vines.
Na kulingana na mchambuzi Eguegu, jambo muhimu limo katika mazowea na Erdogan, katika manufaa yanayoonekana ambayo mataifa ya Afrika yamepata wakati wa uongozi wake.
Mchambuzi wa Kituruki Nebahat Tenriverdi anasema wasiwasi mkubwa zaidi kwa Afrika kuhusu uchaguzi wa Jumapili nchini Uturuki unahusiana na hali ambapo serikali ya Uturuki baada ya Erdogan haitaiweka Afrika juu ya ajenda yake ya sera ya kigeni.
Jambo moja ambalo ni la uhakika ni kwamba Uturuki haitarudi nyuma kwenye mbinu ya zamani ya mtazamo wa ndani.
Soma pia: Rais Erdogan afanya ziara ya kihistoria DRC
Badala yake, upinzani unaonekana kuvutiwa na dhana mpya ya sera ya kigeni yenye jukumu na utambulisho mpya ambao utaongoza kanuni za sera ya kigeni ya nchi hiyo barani Afrika, na pia katika maeneo mengine ambako Uturuki inashiriki, anasema Tanriverdi.
Licha ya utata huo, mchambuzi huyo ana hakika kwamba yeyote atakaeongoza Uturuki, suala muhimu zaidi litakuwa kufufua uchumi, na kwa serikali yoyote ya Ankara itakuwa makini kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Uturuki na Afrika.
Mkakati wa Afrika utaendelea
Kulingana na Tanriverdi, mauzo ya Uturuki barani Afrika na uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni katika nchi kadhaa za Afrika havipaswi kuchukua nafasi ya washirika wa jadi wa kiuchumi wa Ulaya na Marekani. Lakini Afrika inaonekana kutoa uwiano kwa masoko mengine ya kikanda ya Uturuki.
Soma pia: Erdogan aahidi ushirikiano wenye manufaa kwa Afrika
Kwa mfano, baada ya vuguvugu la mataifa ya Kiarabu, wakati Uturuki ilikuwa na matatizo na nchi jirani za Kiarabu, soko la Afrika liligeuka lengo jipya la wafanyabiashara wa Uturuki. Vivyo hivyo, vita vya Ukraine viliamsha maslahi ya kiuchumi barani Afrika, anasema Tanriverdi: "Kuongezeka kwa ushawishi wa Uturuki barani Afrika hakuna ubishi."
Afrika pia inazidi kuwa muhimu kwa makampuni madogo na ya kati ya Uturuki na kwa maeneo ya viwanda kama Gaziantep na Mersin, anasema mchambuzi huyo, akisisitiza: "Bila kujali mabadiliko ya serikali mjini Ankara, nguvu ya Afrika katika uhusiano wa kigeni itabaki."
Mwandishi: Martina Schwikowski