Uturuki, Iran na Uturuki kusuluhisha mzozo wa Syria
5 Aprili 2018Taarifa ya pamoja iliyotolewa na rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, rais wa Iran, Hassan Rouhani, na rais wa Urusi, Vladimir Putin, ilisema viongozi hao wameamua kuongeza jitihada kuhakikisha utulivu unarejea Syria.
Rais Erdogan alisema jeshi lake halitaacha kujaribu kuwafukuza wapigananji wa Syria wenye asili ya Kikurdi kutoka eneo la kaskazini mwa Syria, alipokutana na viongozi wa Urusi na Iran kwa mazungumzo kuhusu njia za kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Syria.
Mataifa hayo matatu, ambayo yameungana kufanya kazi pamoja kutafutua suluhisho la kudumu Syria licha ya tofauti zao, yamesisitiza kujitolea kwao kwa dhati kuulinda uhuru wa Syria na kuendeleza usitishaji wa mapigano nchini humo. Viongozi hao watatu wameitolea wito jumuiya ya kimataifa kutoa msaada zaidi kwa ajili ya Syria.
Erdogan, Putin na Rouhani walifanya mkutano wao wa pili kujadili mustakabali wa Syria, tangu walipohudhuria mkutano kama huo katika mji wa Sochi nchini Syria mwezi Novemba mwaka uliopita. Erdogan alisema vikosi vya Uturuki, ambavyo mwezi uliopita viliidhibiti ngome ya Afrin kaskazini magharibi mwa Syria, vitasonga mbele upande wa mashariki kuelekea mji wa Manbij na maeneo mengine yanayodhibitiwa na kundi la wapiganaji wa Kikurdi, YPG, linaloungwa mkono na Marekani, na ambalo Uturuki inalichukulia kuwa la kigaidi.
"Wanaopata hasara kutokana na mzozo na mapigano ni raia wa Syria. Sote twafahamu fika ni nani atakayeshinda. Kuna ugumu katika siku zijazo, lakini njia ya kutokea inazidi kujitokeza kadri tunavyoendelea kujiimarisha kupata ufanisi."
Uturuki na Urusi kujenga hospitali Syria
Erdogan alisema majeshi ya Uturuki na Urusi yanajadiliana juu ya uwezekano wa kujenga hospitali katika mji wa Tal Abyad nchini Syria kwa lengo la kuwahudumia watu waliojeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa Ghouta Mashariki, kitongoji cha mji mkuu wa Syria, Damascus. Kiongozi huyo wa Uturuki pia alizungumzia mipango ya kujenga maeneo ya kuoka mikate kusaidia kuwapa chakula raia wanaohitaji msaada.
Kwa upande wake rais wa Iran, Hassan Rouhani, alisema alifurahishwa sana wakati Uturuki, Iran na Urusi zilipokubaliana kuwasaidia na kuwaokoa watu wanaoteswa nchini Syria.
"Nchi zote tatu zinataka kutanua msaada ambao zimekuwa zikitoa. Tuendelee kufanya hivyo ili tuwasaidie raia wa Syria wanaokandamizwa pamoja na wale wanaohitaji matibabu. Kwa mtizamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo wa Syria na lazima tuvimalize vita nchini Syria."
Mkutano huo wa pande tatu ulifanyika wakati Marekani ilipotangaza tume yake ya kukabiliana na kundi la dola la kiislamu nchini Syria inafika mwisho, lakini haikutaja tarehe itakapowaondoa wanajeshi wake wapatao 2,000 walioko Syria kama sehemu ya muungano unaoongozwa na Marekani kupambana na kundi la dola la kiislamu tangu 2014. Awali rais wa Marekani Donald Trump, alisema lengo kuu la Marekani lilikuwa kuwashinda wapiganaji wa kundi hilo na walikuwa wanakaribia kulifikia.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Marekani kuondoka Syria, rais wa Iran, Rouhani, alisema hatua hiyo ni kisingizio cha kutafutia fedha kutoka mataifa wanayotaka yaendelee kubakia Syria.
Mwandishi: Josephat Charo/afpe/ap/dpa/reuters
Mhariri: Iddi Sessanga