Uturuki, Iraq kukabiliana na IS baada ya Marekani kujiondoa
3 Januari 2019"Ni jambo muhimu kushirikiana ili tufanikiwe kwenye vita vyetu dhidi ya ugaidi," Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki aliwaambia waandishi wa habari kwenye mkutano wa pamoja kati yake na Rais Barham Salih wa Iraq mjini Ankara siku ya Alhamis (Januari 3).
"Tutaimarisha ushirikiano wetu kufikia lengo hili," alisema Erdogan, akiongeza kwamba kundi la IS ni kitisho kwa Uturuki na Iraq.
Pia kiongozi huyo aliapa kuendeleza mapigano dhidi ya chama cha Kurdistan Workers' Party (PKK) ambacho kimepigwa marufuku nchini mwake lakini kinaendesha shughuli zake nchini Iraq, na ambacho serikali mjini Ankara inadai kinafanya uasi ndani ya ardhi yake.
Syria kiini cha mazungumzo
Salih aliwasili Ankara kwa ziara ya kikazi siku ya Alhamis, ikiwa ni safari yake ya kwanza tangu kuapishwa kushika wadhifa huo mwezi Oktoba. Kiongozi huyo alisema pande hizo mbili "zinapaswa kushirikiana bega kwa bega kuutatua mzozo wa Syria" na kwamba kwenye suala hilo "mataifa hayo yanaweza kufikia matokeo mazuri."
Katika miaka ya karibuni, Ankara na Baghdad zimezidisha juhudi za kupambana dhidi ya kundi la IS ndani ya Syria, huku Marekani ikijipanga kuondosha wanajeshi wake nchini humo. Katika mkesha wa Mwaka Mpya, Iraq ilisema ndege zake za kijeshi ziliyashambulia maeneo ya IS ndani ya Syria, huku Uturuki ikipanga kuendeleza mashambulizi dhidi ya kundi hilo "katika siku zijazo", kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Hulusi Akar.
Kwa muda wa wiki nzima sasa, Uturuki imekuwa ikiimarisha vikosi vyake kwenye eneo la mpaka, ingawa hapo nyuma ilikuwa ikiwalenga tu wapiganaji wa PKK kwenye maeneo ya kaskazini mwa Iraq kwenye mashambulizi yake ya ndege.
Licha ya kwamba nafasi ya Salih kisiasa haina nguvu za kiutawala na maamuzi, lakini vyombo vya habari nchini Iraq vimekuwa vikiitaja ziara yake hii mjini Ankara kama sehemu ya jaribio la Baghdad kuendeleza mahusiano mema na majirani zake na pia mataifa yenye nguvu kwenye eneo hilo.
Ziara ya Salih nchini Uturuki ilikuwa ni ya mwisho katika mfululizo wa ziara zake kwenye eneo hilo ambazo zilianza mwezi Novemba kwa kumpeleka Kuwait, Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri. Iddi Ssessanga