Uturuki: Mamia ya wapiganaji wa Kikurdi na IS wauawa Syria
24 Januari 2018Jeshi la Uturuki limesema limewaua wapiganaji wa Kikurdi 260 nchini Syria pamoja na wanamgambo wa Kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS katika siku nne za kwanza za operesheni zake za eneo la Afrin, kaskazini magharibi mwa Syria.
Hakuna uwepo wa IS katika mji Afrin, ambao uko chini ya udhibiti wa kundi la YPG. Shirika la kufuatilia haki za binaadamu la Syria limeelezea mapigano hayo ya Afrin kuwa makali. Shirika hilo limesema raia 28 wameuawa, madai ambayo serikali ya Uturuki inakanusha vikali.
Mashambulizi ya makombora
Jeshi la Utruruki na washirika wake wa Syria hii leo wameendeleza operesheni dhidi ya YPG, ambayo Marekani inaunga mkono katika vita dhidi ya IS, lakini ambayo Uturuki inalishutumu kwa kuwa na mahusiano na Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi – PKK kinachoendesha uasi wa zaidi ya miongo mitatu nchini Uturuki.
Operesheni hiyo ya kijeshi imefungua uwanja mpya wa mapambano katika vita vya Syria vilivyodumu miak saba, ambao huenda ukatanuliwa na kusababisha ugomvi kati ya Uturuki na mshirika wake wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Marekani. Heather Nauert ni msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani "Wakati tuna wasiwasi kuhusu hali ya sasa kaskazini magharibi mwa Syria, nataka kusema wazi pia kuwa Uturki ni mshirika muhimu wa NATO na kama mwanachama wa NATO tunaelewa wasiwasi wa Utruuki kuhusu makundi kadhaa ya kigaidi. Tunaelewa wasiwasi wao kuhusu PKK, kwa hivyo tunafanya mazungumzo na serikali ya Uturuki kuhusu kushughulikia masuala hayo lakini pia kujaribu kuleta utulivu na kuwahimiza wapunguze mivutano".
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema opereseheni hiyo huenda ikasambaa hadi mji wa Manbij katika upande wa mashariki,a mbako wanajeshi wa Marekani wamekita kambi na wapiganaji wa jeshi la Syriala SDF. Alisisitiza wito wa Uturuki wa kuitaka Marekani kukoma kuliunga mkono kundi la YPG.
Sauti za kimataifa
Mpaka sasa, sauti za jamii ya kimataifa kuhusiana na uvamizi wa Uturuki nchini Syria zimenyamazishwa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kujizuia lakini halikulaani hatua hiyo ya kijeshi wala kutaka isitishwe. Rais wa Urusi Vladmir Putin amezungumza na mwenzake wa Uturuki kwa njia ya simu na akaomba uadilifu wa mipaka ya Syria na uhuru wake vihemishimiwe. Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis ameonya kuwa operesheni ya Utruuki inavuruga juhudi za kuiangamiza IS, kitu ambacho Uturuki imekikataa, ikisema kundi hilo la itikadi kali limefurushwa kabisa nchini Syria.
Simu ya Trump
Msemaji wa Ikulu ya White House Sarah Sanders alisema Marekani inataka kuiona Uturuki ikipunguza mvutano, hatua ambayo Rais wa Marekani Donald Trump ataigusia wakati wa mazungumzo ya simu na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan hii leo.
Urusi na Marekani zinaunga mkono pande pinzani katika vita vya Syria, huku Urusi ikuunga mkono utawala wa Rais wa Syria Bashar al-Assad na Marekani kisiasa ikiuunga muungano wa makundi ya upinzani yanayotaka kumuondoa madarakani Assad, ambaye familia yake imeitawala Syria tangu mwaka wa 1971.
Mwandishi: Bruce Amani/ http://bit.ly/2rybsKf
Mhariri: Caro Robi