1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na Marekani wakubaliana kumaliza mzozo

3 Agosti 2018

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Mike Pompeo, pamoja na mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu wamekubaliana kuendelea kujaribu kusuluhisha mivutano iliyopo baina ya mataifa hayo.

USA Mevlut Cavusoglu, Außenminister Türkei & Mike Pompeo in Washington
Picha: Reuters/L. Millis

Hata hivyo wakati wakikubaliana hayo taarifa zimeeleza kwamba wameshindwa kupata suluhu ya mzozo wa kidiplomasia kuhusu mchungaji wa Kimarekani anayeshikiliwa nchini Uturuki. 

Pompeo alikutana na Cavusoglu pembezoni mwa mkutano uliokutanisha mawaziri wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN, unaofanyika nchini Singapore. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Heather Nauert, aliarifu kwamba mawaziri hao walizungumzia masuala kadhaa na kwamba mazungumzo yao yalikuwa ni yenye kujenga. Wizara hiyo imesema walikubaliana kuendelea kusaka suluhu ya mivutano baina yao.

Kwa upande wake, baada ya mkutano huo Cavusoglu aliwaambia waandishi wa habari kwamba alirejelea ujumbe wa Uturuki kwamba lugha za vitisho na vikwazo hazitasaidia kupatikana mafanikio yoyote, na kwa hiyo yeye na Pompeo watachukua hatua za kusuluhisha tofauti zao wakati watakaporejea nyumbani.

Marekani iliwawekea vikwazo mawaziri wawili wa Uturuki, kutokana na hatua ya Uturuki ya kumuweka kizuizini mchungaji wa Kimarekani, Andrew Brunson, kwa tuhuma za kusaidia ugaidi. Uturuki, hata hivyo, imesema vikwazo hivyo havikubaliki.

Mchungaji Andrew Brunson, ambaye kifungo chake kimesababisha mvutano mkubwa kati ya Marekani na UturukiPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/E. Tazegul

Pompeo aliwaambia waandishi wa habari walioambatana naye nchini Singapore kwamba Marekani imekwishaileza Uturuki kwamba muda unayoyoma na ni wakati wa mchungaji Brunson kurejeshwa nyumbani.

Marekani yataka na raia wake wengine kuachiwa na Uturuki.

Amesema mbali ya Brunson, Wamarekani wengine pia wanaoshikiliwa na serikali ya Uturuki wanapaswa kuachiliwa na kurejea nyumbani. Pompeo ameongeza kuwa watu hao ambao hawana hatia yoyote wamekuwa wakishikiliwa kwa muda mrefu, na kuahidi kuwa watashirikiana kuona kama wanaweza kupata muafaka.

Marekani imekuwa ikiomba kuachiliwa kwa watumishi watatu walioajiriwa na ubalozi wake na hivi sasa wanashikiliwa nchini Uturuki. Waziri Pompeo alisema kabla ya mazungumzo baina yao kwamba Marekani ilikuwa ikimaanisha ilipotaka kuachiwa huru kwa mchungaji huyo.

Brunson, aliyekuwa akiongoza kanisa la Kiprotestanti katika mji wa Izmir, wiki iliyopita alihamishiwa kwenye kifungo cha nyumbani kufuatia kifungo cha miaka miwili jela kwa tuhuma za ujasusi na kuunga mkono makundi ya ugaidi.

Uturuki imetishia kulipiza kisasi kwa hatua ya vikwazo ya Marekani dhidi ya mawaziri wake wawili - wa mambo ya ndani na sheria - kufuatia mvutano huo, na iwapo mchungaji huyo akutikana na makosa, atakabiliwa na kifungo cha miaka 35 jela.

Kesi ya Brunson imekuwa ikifuatiliwa na Rais Donald Trump wa Marekani, pamoja na makamu wake Mike Pence, mwenye uhusiano mkubwa na na jamii ya Kikristu ya Evanjilisti. Kulingana na msaidizi wake, Pence amekuwa akifuatilia uendeshwaji wa shauri hilo tangu Brunson alipokamatwa na amekuwa akishinikiza chini kwa chini kuchukuliwa hatua.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef