Uturuki na Qatar zasitisha upatanishi wa Lebanon
20 Januari 2011Baada ya siku mbili za mazungumzo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki na Qatar, Ahmet Davutoglu na Sheikh Hamad bin Jassem bin Jaber al-Thani, wamesema kwamba kwa sasa wanasitisha juhudi zao za upatanishi.
Hii inafuatia hatua ya jana (19 Januari 2011) ya Saudi Arabia, ambayo pamoja na kujitoa kwenye mazungumzo haya ilionya hatari ya kugawika kwa taifa la Lebanon lenye mchanganyiko wa dini na madhehebu tafauti.
Mkwamo mpya?
Davutoglu na al-Thani wamesema kwamba wanaodoka Beirut baada ya mazungumzo yao na upande wa Hizbullah na ule Saad Hariri, kukumbwa na vikwazo visivyoweza kusawazika kwa sasa.
"Jitihada zetu za mwanzo zilipelekea kuwa na rasimu ambayo inazingatia matakwa ya kisiasa na kisheria kutatua mgogoro uliopo kwa kuegemea msingi ulioanzishwa na Saudi Arabia na Syria, lakini kutokana na masuala kadhaa, tumeamua kusitisha mchakato huu na kurudi kwa viongozi wetu kwa mashauriano zaidi." Walisema katika taarifa yao ya pamoja kwa vyombo vya habari.
Kile kinachoitwa kuwa ni msingi wa Saudi Arabia na Syria, unataka Lebanon iikane mahakama ya Umoja wa Mataifa kuchunguza mauaji ya mwaka 2005 ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Rafiq Hariri, kwa upande mmoja, na kundi la Hizbullah kutoa uhakikisho wa kuweka wazi silaha zake kwa upande mwengine. Pia unataka pawepo na hakikisho la kufanya kazi kwa taasisi za serikali.
Mpango wa Saudi Arabia na Syria
Kwa mujibu wa vyanzo vya kisiasa, rasimu ya mpango huu iliwasilishwa kwa Hizbullah usiku wa jana na Davutoglu na al-Thani, lakini maafisa wa Hizbullah wamekataa kuzungumzia lolote kuhusiana na hili.
Akizungumza na Shirika la Habari la AFP, mbunge wa chama cha Saad Hariri, Atef Majdalani, amesema kwamba, sasa Hizbullah inaonekana kupendelea zaidi njia za kijeshi kulazimisha ajenda yake.
"Kwa kiasi ninachoelewa, ni kuwa kwa kuondoa mawaziri wake serikali, Hizbullah ilikuwa imeshakusudia kutumia njia za kijeshi kufanya mapinduzi, lakini wajuwe kuwa hatua hiyo itamaanisha mwanzo wa mwisho wao." Amesema Majdalani.
Lebanon ipo kwenye mgogoro mkubwa kati ya serikali ya Saada Hariri, ya mtoto wa marehemu Rafiq Hariri, ambayo inaungwa mkono na Marekani na Saudi Arabia na chama cha Hizbullah, ambacho kinaungwa mkono na Syria na Iran, juu ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya Rafiq Hariri.
Juzi Jumatatu (18 Januari 2011), mwendesha mashtaka wa Mahakama hii Maalum, aliwasilisha hati ya mashtaka, ambayo sasa inahakikiwa na jaji. Hizbollah imesema kwamba hati hiyo ina majina ya wanachama wake, na inatuhumu kuwa hiyo ni njama ya Marekani na Israel dhidi yake. Chama hiki, chenye uugwaji mkubwa wa jamii ya Kishia, kina nguvu kubwa za kijeshi na pia za kisiasa, na kujitoa kwake kwenye serikali wiki iliyopita, kulisababisha kuporomoka kwa serikali iliyokuwa ikiongozwa na Saad Hariri.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman