1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na Urusi wakubaliana kusitisha machafuko Idlib

Josephat Charo
12 Machi 2020

Maafisa wa Uturuki na Urusi wamekubaliana kuhusu kusitisha mapigano katika eneo la Idlib. Makubaliano hayo yamefikiwa huku kukiwa na taarifa za kuuliwa wapiganaji 26 mashariki mwa Syria.

Türkei Hatay Verteidigungsminister Hulusi Akar
Picha: picture-alliance/AA/A. Akdogan

Makubaliano hayo yameafikiwa kwenye mazungumzo yaliyofanyika mjini Ankara. Waziri wa ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar alinukuliwa na chombo cha habari cha taifa Anadolu akisema kwa kiwango kikubwa Uturuki na Urusi wamekubaliana kuhusu vipengee muhimu kuhusu usitishwaji wa mapigano huko Idlib.

Akar alisema mazungumzo na Warusi bado yanaendelea na kwamba wanajeshi wa Uturuki wameendelea kubakia katika maeneo yao Idlib. Pia amesema Uturuki itaendelea na harakati yake ya kijeshi Idlib iwapo makubaliano ya kusitisha mapigano hayataheshimiwa. Waziri Akar alisisitiza onyo lililotolewa na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan siku moja kabla.

Erdogan ameapa kuwa jeshi la Uturuki litachukua hatua kali kama serikali ya Syria itakiuka mkataba wa kusitisha mapigano katika mkoa wa Idlib.

Wiki iliyopita viongozi wa Uturuki na Urusi walikubaliana kuhusu mkataba uliolenga kusitisha machafuko Idlib. Mkataba huo unaoziunga mkono pande zinazohasimiana katika mzozo huo, ulisaidia kusitisha operesheni ya serikali ya Syria ya mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya ngome ya mwisho ya waasi mkoani Idlib iliyodumu muda wa miezi mitatu. Mamia ya watu waliuliwa katika operesheni hiyo na wengine milioni moja kulazimika kukimbilia eneo la mpakani na Uturuki.

Mwanamume wa Syria akihesabu pesa katika kituo cha kubadilisha fedha mjini Binnish mkoani IdlibPicha: Getty Images/AFP/M. Haj Kadour

Ujumbe wa Urusi uliwasili mjini Ankara wiki hii kujadili vipengee vya mkataba huo, ikiwemo ukanda wa usalama na doria za pamoja katika barabara kuu muhimu ya M4.

Wapiganaji kutoka Iraq wauawa

Mapatano haya yaliafikiwa wakati wapiganaji 26 kutoka Iraq wakiuliwa mashariki mwa Syria. Shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, lilisema wapiganaji hao wa kundi la Hashed al-Shaabi wameuawa kwenye shambulizi la kutokea angani lililofanywa na wanajeshi wa muungano unaongozwa na Marekani nchini Iraq.

Likitoa takwimu mpya za vifo leo kufuatia shambulizi hilo karibu na mji wa mpakani wa Albu Kamala jana, shirika hilo lilisema huenda hujuma hiyo ilifanywa na muungano unaoongozwa na Marekani unaopambana na kundi linalojiita dola la kiislamu IS.

Makubaliano kati ya Uturuki na Urusi yalijiri wakati mzozo wa Syria ukiingia mwaka wa kumi leo huku matumaini ya kupatikana suluhu yakiendelea kufifia. Miaka tisa tangu mzozo huo kuanza mnamo mwezi Machi 2011 rais wa Syria Bashar al Assad bado yupo madarakani na ataendelea kuwepo, huku zaidi ya watu 380,000 wakiwa wameuliwa. Miji mingi ya Syria imeharibiwa kabisa na nusu ya idadi jumla ya wakazi wamelazimika kuyahama makazi yao na kuishi katika maeneo mengine ndani au nje ya nchi yao.

ape/afpe

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW