Uturuki, NATO na Marekani zakutana kuhusu IS
9 Oktoba 2014Viongozi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na Marekani wanakutana leo na maafisa wa Uturuki ili kujadaliana kuhusu mkakati wa kijeshi ili kusaidia kuwazuia wanamgambo hao dhidi ya kuutwaa mji wa Kobani. Pande zote zinahofia kuwa mji huo unakaribia kuanguka mikononi mwa IS, lakini zinatofautiana kuhusu namna ya kuwasaidia wapiganaji wa Kikurdi wanaopambana ndani ya mji huo.
Mkutano huo wa siku mbili unaanza leo mjini Ankara, ambapo maafisa wanatarajiwa kujadili kuhusu kitisho cha Dola la Kiislamu kwa usalama wa Uturuki. Akizungumza baada ya mkutano na Katibu Mkuu mpya wa NATO Jens Stoltenberg, Waziri wa Mambo ya Kigeni Mevlut Cavusoglu, amesema Uturuki haiwezi kuchukua hatua kivyake.
Stoltenberg baadaye atazungumza na rais wa Uturuki, waziri mkuu na waziri wa ulinzi. Marekani pia imewatuma wajumbe kadhaa kushiriki katika mazungumzo hayo.
Katikati ya mwezi Septemba, IS ilianzisha mashambulizi katika mji wa Syria, Kobane, ambao uko karibu na mpaka wa Uturuki. Wakurdi wamekuwa wakijaribu kuulinda mji huo, lakini hata wakati Marekani ikiendelea kuyalipua na kuharibu maeneo ya IS, mapambano ya udhibiti wa mji huo yanaonekana kuvunjika.
Rais wa Marekani Barack Obama alijadiliana na makamanda wanaoongoza mashambulizi dhidi ya IS wakati jeshi la Marekani likionya kuwa mashambulizi ya kutokea angani pekee hayawezi kulizuia kundi hilo dhidi ya kuutwaa mji huo muhimu wa Syria. Akizungumza katika mkao makuu ya ulinzi - Pentagon, Obama alisema haitakuwa rahisi kulishinda kundi la IS lakini akasema kuwa muungano wa kimataifa unajitahidi kupambana na wanamgambo hao wa Kisunni wenye msimamo mkali wanaoyateka maeneo ya Iraq na Syria.
Uturuki imeweka vifaru vyake katika eneo la mpaka karibu na mji wa Kobane, lakini hatua yoyote ya kijeshi inayochukuliwa. Rais Recep Tayyip Erdogan ametoa wito kwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kuyapeleka mjini humo majeshi ya ardhini. Akisema kuwa kudondosha mabomu kutokea angani siyo suluhisho.
Erdogan kufikia sasa amekataa kujiunga na operesheni hiyo inayoongozwa na Marekani bila kupewa ahadi na Marekani kuwa pia itachukua hatua dhidi ya rais wa Syria Bashar al-Assad. Wizara ya Ulinzi hata hivyo imeondoa uwezekano wa kuyapeleka majeshi ya ardhini hasa baada ya operesheni za kijeshi zilizoshindwa kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali nchini Afghanistan na Iraq.
Wakati huo huo,waandamanaji wa Kikurdi wanaokarishwa na hatua ya serikali ya Uturuki kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wapiganaji wa jihadi nchini Syria wamekabiliana na polisi kwa usiku wa tatu mfululizo huku idadi ya vifo kutokana na vurugu hizo ikiongezeka hadi waru 22.
Huku wakikiuka amri ya kutotoka nje iliyotangazwa na jeshi, mamia ya waandamanaji waliingia barabatani katika miji ya Kikurdi kusini mashariki mwa Uturuki na wakatawanywa na polisi waliotumia mabomu ya kutoa machozi na mizinga ya maji.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Josephat Charo