Uturuki, Urusi na Iran wakubaliana kuhusu katiba ya Syria
17 Septemba 2019Hii ni kama sehemu ya suluhisho la kisiasa katika vitavya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo ambavyo kwa sasa vimeingia mwaka wa tisa.
Baada ya mkutano uliowaleta pamoja marais hao watatu mjini Ankara, Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan amesema kwamba tofauti kuhusiana na mwanakamati mmoja wa mwisho zimetatuliwa jambo linalotoa nafasi kwa kamati hiyo kuanza kufanya kazi hivi karibuni.
"Tumeonyesha nia nzuri ya kutambua wanakamati na sheria zitakazotumika. Tumefanya juhudi za mchakato wa kisiasa kusonga mbele. Kwa ufupi vikwazo vilivyokuwa vinazuia kubuniwa kwa kamati vimeondolewa na juhudi zetu," alisema Erdogan.
Viongozi hao wana wasiwasi kuhusiana na hali mashariki mwa Euphrates
Viongozi hao hawakutoa muda maalum wa kamati hiyo kuanza shughuli zake. Kamati hiyo itajumuisha maafisa kutoka serikali ya Syria na upinzani. Viongozi hao wamesema wana wasiwasi kuhusiana na uwezekano wa hali ya kibinadamu kuendelea kuwa mbaya ndani na nje ya eneo la Idlib na wamekubaliana kuchukua hatua kuzuia kukiukwa kwa makubaliano ya awali kati ya nchi hizo tatu.
"Tuna wasiwasi kuhusiana na hali mashariki mwa mto Euphrates. Hali inasalia kuwa mbaya. Tunaelewa umuhimu wa Jamhuri ya Syria kuweka hadhi ya mpaka wake na majirani zake - hapa nazungumzia haki za kisheria za nchi jirani ikiwemo Uturuki kuweka usalama wa mpakani," alisema Rais Vladimir Putin.
Rais Putin pamoja na mwenzake wa Iran Hassan Rouhani wamekuwa wakimuunga mkono Rais wa Syria Bashar al-Assad dhidi ya waasi wakati ambapo Erdogan pamoja na Marekani na Ulaya na marafiki wake wa nchi za Kiarabu wamekuwa wakiungo mkono makundi tofauti ya waasi.
Taarifa hiyo haikuzungumzia kuhusu mashambulizi yaliyofanywa Saudi Arabia
Erdogan vile vile amesema kuwa wanapanga kubuni "eneo salama" pamoja na Urusi na Iran kaskazini mwa Syria ambalo amesema huenda likawa makao ya karibu wakimbizi milioni tatu ambao kwa sasa wanaishi Uturuki.
Taarifa hiyo ya pamoja lakini haikuyataja mashambulizi ya Jumamosi katika visima viwili vya mafuta vya kampuni ya Saudi Arabia ya Aramco yaliyofanywa na waasi wa Houthi walioko nchini Yemen ambao wanaungwa mkono na Iran. Saudi Arabia inasema mashambulizi hayo yalifanywa kwa kutumia silaha za Iran.
Lakini Rais Hassan Rouhani amesema mashambulizi hayo yalifanywa na Wayemen kama kulipiza kisasi cha mashambulizi yanayofanywa nchini mwao.