1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaapa kupambana na Magaidi

2 Januari 2017

Mamlaka nchini Uturuki zimeanzisha msako mkali kumtafuta mtu aliyetekeleza mashambulizi katika klabu ya usiku na kuuwa watu wapatao 39.

Türkei Anschlag Istanbul
Picha: Reuters/O.Orsal

Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan amekapa kuwa hawatasalimu amri kwa watu ambao wanataka kupandikiza machafuko. Wakati huo huo vyombo vya habari vinaripoti kuwa kundi linalojiita dola la kiislam IS limedai kuhusika na mashambulizi  hayo.

Mamlaka zinaamini kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alishambulia na kuuwa watu, wengi wao wakiwa ni raia wa kigeni anatokea kati ya nchini Uzebekistan au Kyrgyzstan mataifa yaliyo Asia ya kati.

Mshambuliaji huyo ambaye mpaka sasa hajulikani alipo, akiwa nje ya klabu inayofahamika kwa jina la Reina saa za alfajiri za  mwanzo mwa 2017, alianza kwa kumshambulia kwa risasi askari polisi na mtu mmoja waliokuwa nje ya ukumbi kabla ya kuingia ndani na kuanza kuwafyatulia risasi watu karibu 600 waliokuwa wakisherehekea ukumbi hapo.

Polisi imeendelea na uchunguzi kutaka kufahamu kama IS ilihusika pia na mashambulizi ya bomu la kujitoa mhanga na mashambulizi ya silaha yaliyofanyika mwezi Juni mwaka jana katika kiwanja cha ndege ya Ataturk mjini Instanbul, kufuatia kuwepo kwa matukio ya kufanana na tukio hilo.

Baadhi ya polisi waliozingira eneo kulipofanyika mashambuliziPicha: Reuters/O.Orsal

Mashambulizi hayo yanafuatia zaidi ya matukio 30 ya kikatili yaliyotokea mwaka jana nchini Uturuki, nchi ambayo pia ni mwanachama wa jumuiya ya kujihami NATO na mshirika wa muungano unaaongozwa na Marekani wa kupambana na kundi la IS nchini Syria na Iraq. Uturuki imeshambuliwa kwa mabomu mara kadhaa mwaka 2016, mashambulizi matatu yakiwa yamefanyika katika mji wa Instanbul IS inashukiwa kuhusika.

Esref Kocar ni mkazi wa mjini Instabul  amesema anasikitishwa kwa kiasi kikubwa kuona kuwa Uturuki inakuwa na habari kuhusu matukio ya kigaidi na kuongeza kuwa hakuna kizuri au kibaya katika ugaidi, ugaidi ni mbaya. "Hakuna maelezo mengine, aibu kwao walioamuru kufanyika kwa tukio hilo".

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani mashambulizi hayo, katika taarifa yake, wajumbe wa baraza hilo wamesema shambulio hilo ni la kigaidi na la kutisha na kisha kusisitiza kuwa kila matukio ya kigaidi ni uhalifu usiokuwa na msamaha bila kujali msukumo wake, wakati wowote, popote na mtu yoyote ambaye atatekeleza.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/DPA/AP

Mhariri:Iddi Ssessanga