1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaikosoa Ujerumani kuhusu Libya

Josephat Charo
7 Agosti 2020

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, amesema hatua ya Ujerumani kushiriki katika tume ya vikwazo vya silaha ya Umoja wa Ulaya ya Irini, ina maana serikali ya mjini Berlin inaegema upande mmoja. 

Libyen Konflikt Symbolbild ARCHIV
Picha: AFP/M. Turkia

Akizungumza jana Alhamisi waziri Cavusoglu aliukosoa ushiriki wa Ujerumani katika tume ya Umoja wa Ulaya inayosimamia utekelezaji wa kikwazo cha silaha cha kimatafa dhidi ya Libya. Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Uturuki alikuwa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa mazungumzo na Fayez al Sarraj, waziri mkuu wa serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Uturuki ni mojawapo ya nchi zinazoinaiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa ya Tripoli.

Katika kauli alizozitoa kwa vyombo vya habari vya Uturuki baada ya mkutano huo, Cavusoglu aliituhumu Ujerumani kwa kuudhoofisha uwezo wake wa kutofungamana na upande wowote katika mgogoro wa Libya baada ya Ujerumani siku ya Jumanne kutuma kikosi chake cha wanajeshi 250 kushiriki katika tume ya Umoja wa Ulaya ya Irini.

Tume hiyo ilizinduliwa mnamo mwezi Mei mwaka huu kwa lengo la kuzuia silaha kuingia Libya, taifa ambalo limegubikwa na mvutano mkubwa wa kung'ang'ania madarakaka kati ya serikali ya umoja wa kitaifa mjini Tripoli na vikosi tiifu kwa kamanda wa jeshi la mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar.

Cavusoglu ameliambia shirika la habari la serikali ya Uturuki, Anadolu, kwamba tume ya Irini ina upendeleo na Ujerumani kama mwenyeji wa mkutano wa Berlin, inatakiwa isifungamane na upande wowote wala kuwa na upendeleo.

Hatua ya Ujerumani yauzidisha makali mgogoro

Mwezi Januari mwaka huu Ujerumani iliandaa mkutano wa kimataifa uliojadili mgogoro wa Libya ambapo nchi kadhaa zilikubaliana kuendeleza kikwazo cha silaha dhidi ya Libya.

Mevlut Cavusoglu, kulia, na Sarraj mjini TripoliPicha: picture-alliance/AP/Turkish Foreign Ministry/F. Aktas

Cavusoglu amesema ushiriki wa Ujerumani katika tume ya Irini itauondolea uhalali mkutano huo wa Berlin na maazimio yaliyoafikiwa. Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki pia amesema hatua hiyo inauchochea zaidi mzozo wa Libya na kuifanya hali kubwa ngumu zaidi kuliko ilivyo sasa.

Cavusoglu amehoji kuwa tume ya Irini inavipendelea vikosi vya kamanda Haftar. Aliwahi mwezi Juni kuikosoa tume hiyo kwa kuegemea upande mmoja na kushindwa kuvilenga vifaa vya kijeshi vinavyotokea kwa wafuasi wa Haftar.

Uungwaji mkono wa kimataifa kwa serikali ya umoja wa kitaifa mjini Tripoli na vikosi vya Haftar umegawanyika, huku Ufaransa ikionekana kumuunga mkono Haftar pamoja na Misri, Syria, Urusi na Umoja wa Falme za Kiarabu. Uturuki inaisaiia kijeshi serikali ya umoja wa kitaifa ya Tripoli, zikiwemo ndege zinazoendeshwa bila rubani zilizosaidia kuwafurusha wapiganaji wa Haftar kutoka eneo la kaskazini magharibi.

Mgawanyiko katika uungwaji mkono wa kimataifa kwa pande mbili zinazohasimiana Libya umesababisha mtihani mkubwa katika kuutanzua mgogoro uliopo na umeifanya kuwa vigumu kutekeleza kikwazo cha silaha cha Umoja wa Mataifa dhidi ya Libya.

(dpa,afp)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW