1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yailaumu EU von der Leyen kukosa kiti mkutanoni

Angela Mdungu
8 Aprili 2021

Uturuki imeugeuzia kibao na kuutupia lawama umoja wa Ulaya EU kutokana na mpangilio wa ukaaji uliomwacha Rais wa halmashauri kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen bila kiti katika mkutano wake na Rais Recep Tayyip Erdogan

Türkei | EU Delegation in Ankara
Picha: EU Delegation Turkey

Rais Erdogan alijikuta akikosolewa vikali baada ya kusambaa kwa picha ya mkutano wake na Von der Leyen pamoja na Rais wa baraza la Ulaya  Charles Michel uliofanyika mjini Ankara Jumanne wiki hii. Katika chumba walichokuwa wamekaa viongozi hao watatu kulikuwa na viti viwili pekee vilivyokuwa vimepangwa sambamba na bendera za Umoja wa Ulaya na Uturuki.

Erdogan na Michel walikaa haraka kwenye viti vyao wakati Von der Leyen ambaye cheo chake kwa protokali za kidiplomasia ni sawa na za viongozi hao wawili wa kiume alibaki akiwa amesimama. Baadaye, picha rasmi zilimuonesha akiwa amekaa kwenye Sofa akitizamana na waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu.

Katika kauli yake ya kwanza kutolewa na Uturuki kuhusu mpangilio huo wa ukaaji Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Uturuki amesema mpangilio ulipangwa kulingana na pendekezo la Umoja wa Ulaya. Amesema wasingefichua ukweli huo kama kusingekuwa na tuhuma dhidi ya Uturuki.

Ukosolewaji mkali twitter

Sakata hilo la kidiplomasia lilishika kasi twitter na kupewa jina la "sofagate" ambapo lilizua gumzo na kuwa sehemu ya mjadala wa mwanzo wa mkutano wa Uturuki na Umoja wa Ulaya. Viongozi hao watatu walikutana katika juhudi za kuboresha mahusiano baada ya miezi kadhaa ya msuguano. Hata hivyo mazungumzo hayo yaliishia kwa maafisa wa Ulaya kulaumu mfumo dume ambapo wamemuunganisha Rais Erdogan na kujitoa kwa nchi yake katika azimio dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Charles Michel, Recep Tayyip Erdogan, Ursula von der LeyenPicha: Murat Kula/AA/picture alliance

Makundi kadhaa ya bunge la Umoja wa Ulaya yametaka uchunguzi ufanyike kuhusu namna ambavyo  von der Leyen alivyoachwa bila kiti huku Michel akiwa amekaa. Mjumbe wa bunge la Ulaya wa Ubelgiji Assita Kanko ametuma swali rasmi kwa Rais wa baraza la Ulaya Charles Michel, akisema kuwa mpangilio katika mkutano huo haukuzingatia mtiririko wala cheo bali  mfumo dume unaowakilisha udikteta.

Kwa upande wake, msemaji wa Von der Leyen, Eric Mamer, alikataa kuruhusu hisia juu ya namna mkanganyiko huo ulivyotokea  kwa kuwa Tume ya Ulaya haijawahi kutuma timu ya maandalizi mjini Ankara. Amesema, hayo ni mambo ya ndani ya Umoja wa Ulaya na kwamba Von der Leyen anataka maswali hayo yatafakariwe ili hali hiyo isijitokeze katika shughuli zijazo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW