1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaishutumu Saudi Arabia

Isaac Gamba
12 Oktoba 2018

Vyombo vya habari vya Uturuki vimeripoti kuwa maafisa wa Uturuki wanasauti na picha zilizorekodiwa zinazothibitisha kuwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi aliuawa mapema mwezi huu Oktoba.

Jamal Khashoggi
Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

 

Kwa mujibu wagazeti la Washington Post Serikali ya Uturuki inazo picha za vidio pamoja na sauti zinazothibitisha kuwa Jamal Khashogi aliuawa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul  mapema mwezi huu.

Ikiwakariri maafisa kadhaa wa Marekani pamoja na Uturuki ambao taarifa hiyo inasema picha na sauti zilizorekodiwa zinaonesha Khashoggi ambaye ni mwandishi wa habari na mkazi wa Marekani alihojiwa, kuteswa na baadaye kuuawa baada ya kuingia ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mnamo Oktoba 2 kufanya matayarisho ya ndoa yake.

Akizungumzia tukio hilo mwandishi wa habari na rafiki wa karibu wa Khashoggi, Azzam Tamimi anasema:

Uturuki inaishutumu Saudi Arabia kwa kumuua Khashoggi na kuondoa mwili wake katika ubalozi huo mdogo.

Jumatano wiki hii vyombo vya habari vya Uturuki vilitoa vidio ya kamera ya usalama inayodaiwa kuwa ya kikosi cha mauaji kinachotuhumiwa kumua Jamal Khashoggi. Vidio hiyo haioneshi picha kamili au matukio ndani ya ubalozi.

Maafisa wa Marekani na Uturuki wamezungumzia taarifa za vidio hiyo wakisema kundi la wanaume 15 linaweza kuwa limetumwa kumteka nyara Khashoggi na kumrejesha Saudi Arabia na siyo kumuua.

 

Saudi Arabia yakanusha

Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin AbdulazizPicha: Reuters/Courtesy of Saudi Royal Court/B. Algaloud

Maafisa wa Saudi Arabia wanakanusha vikali iwapo wanajua lolote juu ya suala la Khashoggi ambaye alikuwa karibu na serikali ya Saudi Arabia kabla ya kuanza kuikosoa serikali ya nchi hiyo ya kifalme na Mwanamfalme Mohammad bin Salman.

Alhamisi wiki hii mshauri wa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, Ibrahim Kalin alisema Uturuki na Saudi Arabia waliunda kundi la pamoja kwa ombi la Saudi Arabia ili kuelezea picha halisi kwa pande zote kuhusiana na suala hilo linalomuhusu Jamal Khashoggi.

Wakati hayo yakiendelea utawala wa Rais Donald Trump umekuwa ukisita kuchukua hatua juu ya tuhuma hizo. Trump amejenga ushirikiano madhubuti na mwanamfalme Mohammed ambaye amejitahidi kuonyesha binafisi kuwa yeye ni mwanamageuzi anayefanya juhudi za kulifanya taifa hilo kuwa kivutio cha utaliii.

Jana jioni Trump alisema katika mahojiano kuwa kupotea kwa mwandishi huyo wa habari ni jambo lisilokubalika.

Aidha, Trump amesema haoni sababu ya kusimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia kwa sababu ya kutoweka kwa Khashoggi. Trump amesema Marekani inaweza kusaidia katika uchunguzi ili kubaini kilichomfika Khashoggi ambaye ni mkosoaji maarufu wa sera za Saudi Arabia. Kashoggi alionekana mara ya mwisho akiingia kwenye ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul Oktoba 2. 

Mwandishi: Isaac Gamba/DW/AP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW