1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Uturuki yaitaka dunia kuiunga mkono Azerbaijan

6 Oktoba 2020

Mwanadiplomasia wa juu wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amezuru Baku kuonesha mshikamano na Azerbaijan katika mzozo wake wa miongo kadhaa za Armenia kuhusu eneo lililojitenga la Nagorno-Karabakh, ambako mapigano yanaendelea.

Türkei Mevlut Cavusoglu
Picha: Reuters/Turkish Foreign Ministry

Mapigano makali yalioanza Septemba 27 kati ya vikosi vya Azerbaijan na Armenia katika eneo hilo yamepelekea vifo vya wanajeshi na raia wa pande mbili. Eneo la Nagorno-Karabakh liko ndani ya mipaka ya Azerbaijan lakini limekuwa chini ya udhibiti wa vikosi vya asili Armenia vinavyoungwa mkono na Armenia tangu kumalizika kwa vita vya kujitenga mwaka 1994. Makabiliano yameendelea licha ya miito ya kimataifa ya kusitisha mapigano.

Soma pia:Mapigano yamezuka kati ya Armenia na Azerbaijan 

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amekosoa miito hiyo ya kuwepo na mapatano kati ya nchi hizo mbili na kuitaka jamii ya kimataifa kusimama na Azerbaijan, akisema usitishaji wa zamani wa mapigano ulishindwa kukomesha ukaliaji wa Armenia wa ardhi ya Azerbaijan. Cavusoglu ameishutumu Armenia kwa uhalifu wa kivita kwa kushambulia makaazi ya raia katika maeneo ya makaazi ndani ya Azerbaijan.

Eneo la Nagorno-Kabarakh liko ndani ya Azerbaijan lakini lilivamiwa na kukaliwa na majeshi ya Armenia, miaka 30 iliyopita, kufuatia vita vya kutaja kujitenga.

Soma pia: Mkuu wa NATO ataka mapigano yasitishwe Nagorno-Karabakh

"Tunaangalia miito inayotoka duniani na ni usitishaji mapigano mara moja. Kisha nini? Kulikuwepo na usitishaji uhasama hadi sasa na nini kilitokea? Armenia ilishambulia Tovuz na Azerbaijan ikajibu. Jamii ya kimataifa ilitoa wito wa kusitisha mapigano. Usitishaji mapigano ulitekelezwa, kisha kilitokea nini? Muda mfupi baadae, Armenia ikashaishambulia Tovuz mwezi Septemba - Armenia ikaishambulia tena Azerbaijan. Katika maneno mengine, kunaweza kuwa na usitishaji mapigano lakini matokeo yatakuwaje? Unaweza kuiambia Armenia kuondoka mara moja kwenye ardhi ya Azerbaijan? Unaweza alau kuja na suluhisho la kujiondoa? Hapana."

Soma pia: Mapigano ya Armenia-Azerbaijan yapamba moto

Azerbaijan yaishukuru Uturuki

Mwenzake wa Azerbaijan, Jeyhun Bayramov, amesema wameunga mkono juhudi za suluhisho la amani, lakini Armenia imenufaika na matunda ya ukaliaji kwa miaka 30. Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev, ambaye pia alikutana na Cavusoglu, ameishukuru Uturuki kwa kuiunga mkono Azerbaijan, na kusema msaada huo unawahamasisha na kuwapa nguvu zaidi na wakati huo unatoa mchango muhimu katika kuhakikisha utulivu na ustawi katika kanda hiyo.

Wanajeshi wa Armenia wakifanya doria katika mitaa ya mji mkuu Baku. Mapigano yalizuka kati ya Azerbaijan na Armenia Septemba 27, 2020.Picha: Murad Orujov/Sputnik/dpa/picture alliance

Azerbaijan imesema kwamba kuondoka kwa Armenia katika eneo hilo linalotaka kujitenga ndiyo sharti pekee la kumaliza mapigano. Maafisa wa Armenia wanadai kuwa Uturuki inashiriki katika mzozo huo na kuipatia Azrebaijan silaha na wapiganaji kutoka Syria.

Soma pia: Armenia yakataa upatanishi wa Urusi katika mzozo na Azerbaijan

Rais wa Syria Bashar Al-Assad, pia ametoa madai sawa na hayo katika mahojiano na shirika la habari la Urusi RIA, na kusema Rais wa Uturuki Recept Tayyip Erdogan ndiye mchochezi mkuu na mwanzilishi wa mzozo wa karibuni kati ya Armenia na Azerbaijan, akirejea madai yaliotolewa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwamba Uturuki imetuma mamluki kupigana katika mzozo huo. Hata hivyo, Assad hakuonekana kuwa na ushahidi wa madai yake.

Chanzo: APE, RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW