Uturuki yaitaka Saudi Arabia kuutoa mwili wa Jamal Khashoggi
26 Oktoba 2018Tangazo la rais Recep Tayyip Erdogan linakuja siku moja baada ya muendesha mashitaka huyo wa Saudi Arabia kusema kutokana na ushahidi uliotolewa na Uturuki, mauaji ya Jamal Kashoggi yalipangwa. hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa taifa hilo kutoa tamko kama hilo juu ya mauaji ya hayo.
Kuuwawa kwa Kashoggi tarehe 2 Oktoba mwandishi wa gazeti la Marekani la Washington post na mkosoaji mkubwa wa sera za mrithi wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman maarufu kama MBS kumesababisha lawama kali dhidi ya utawala wa Saudi Arabia.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa wito kwa ufalme wa Saudia kuweka wazi ni nani hasa alieamuru mauaji ya muandishi habari Jamal Khashoggi. "Lazima muoneshe mwili wake," alisema Erdogan wakati alipokuwa anawahutubia wanachama wa chama chake mjini Ankara hii leo.
Mwandishi habari huyo aliekuwa na miaka 59 amekuwa akiishi uhamishoni nchini Marekani tangu mwaka 2017. Aliuwawa baada ya kuingia Ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul tarehe mbili mwezi huu ili kupata stakabadhi aweze kumuoa mchumba wake raia wa Uturuki.
Ujerumani yasema itasimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia mpaka uchunguzi ukamilike juu ya mauaji ya Khashoggi
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameapa kusimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia hadi pale maelezo ya kina yatakapotolewa juu ya mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi.
Nae rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema kusimamisha mauzo hayo kwa sababu ya mauaji ya mwanahabari huyo ni hatua isiyofaa. Kwa sasa falme hiyo imewatia nguvuni maafisa wake 18 wanaoshukiwa kuhusika na mauaji hayo.
Huku hayo yakiarifiwa mtaalamu wa Umoja wa Mataifa Agnes Callamard alisema hapo jana kwamba Kashoggi ni muathirika wa mauaji yalio kinyume cha sheria yaliotekelezwa na Saudi Arabia huku akitaka uchunguzi wa kina kufanyika juu ya suala hilo.
Kulingana na shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, mtotowa kiume wa Mwandishi Jamal Kashoggi Salah Kashaoggi hatimae ameruhusiwa kuondoka nchini Saudi Arabia na kuelekea Marekani baada ya hatua ya kumpiga marufuku kusafiri aliowekewa na falme hiyo.
Kuondoka kwake kulikuja baada ya kuonekana kwenye picha akipeana mkono na mrithi wa Ufalme Mohammed Bin Salman huku akimtazama kwa ujasiri
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman